Aug 13, 2022 01:30 UTC
  • Makumi ya magaidi wauawa kaskazini mwa Nigeria

Kwa akali wanamgambo 29 wameuawa huku wengine wasiopungua 55 wakitiwa mbaroni katika operesheni ya jeshi la Nigeria kaskazini mashariki mwa nchi.

Hayo yamesemwa na Bernard Onyeuko, Msemaji wa Jeshi la Nigeria katika kikao na waandishi wa habari jijini Abuja na kuongoza kuwa, watu 52 waliokuwa wameshikiliwa mateka na magaidi hao wameokolewa kwenye operesheni hiyo.

Onyeuko amebainisha kuwa, katika operesheni hiyo iliyofanyika ndani ya wiki mbili zilizopita, wanachama 1,755 wa kundi la kigaidi la Boko Haram pamoja na jamaa zao wamejisalimisha mikononi mwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Msemaji wa Jeshi la Nigeria ameongoza kuwa, kamanda mwandamizi wa kundi la Daesh tawi la Afrika Magharibi (ISWAP) Alhaji Modu (Bem Bem), pamoja na wapiganaji wake wameuawa katika shambulizi la anga dhidi ya maficho yao katika kijiji cha Degbawa, karibu na Milima ya Mandara, jimboni Borno.

Wanachama wa Boko Haram

Haya yanajiri wakati huu ambapo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria anaendelea kukosolewa kwa kushindwa kukabiliana na magenge hayo ya kigaidi hususan katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa nchi.

Ikiwa imebakia miezi sita tu hadi kufanyika uchaguzi wa rais nchini Nigeria, malalamiko dhidi ya Muhammadu Buhari (79) yamezidi kuwa makubwa.

 

Tags