Aug 13, 2022 11:16 UTC
  • Rais wa Sierra Leone: Maandamano yalioua 27 yalilenga kuipindua serikali

Rais wa Sierra Leone amesema maandamano ya fujo yaliyoshuhidiwa wiki hii nchini humo yalifanyika kwa shabaha ya kuipundua serikali anayoiongoza.

Rais Julius Maada Bio alisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, maandamano hayo ya ghasia yaliyopelekea kuuawa raia 21 na maafisa usalama wasiopungua sita yalikuwa ni sehemu ya jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali.

Akilihutubia taifa, Rais Maada Bio amesema: Haya hayakuwa maandamano ya kulalamikia gharama ya juu ya maisha iliyosababishwa na mgogoro wa kiuchumi unaoshuhudiwa duniani kote.

Amebaiisha kuwa, nara zilizokuwa zikipigwa kwenye maandamano hayo zilikuwa za kuchochea mapinduzi ya fujo dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.

Askari polisi Sierra Leone

Rais wa Sierra Leone amesisitiza kuwa, vyombo vya dola vitachunguza mauaji yote yaliyofanywa kwenye maandamano hayo hususan katika mji mkuu Freetown. Maandamano ya namna hii ni nadra kufanyika katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, hususan jijini Freetown.

Mfumko wa bei za bidhaa nchini humo ulipanda kwa asilimia 28 mwezi Juni, na kuwaongezea matatizo ya kiuchumi na kijamii akthari ya wananchi wa nchi hiyo yenye jamii ya watu milioni 8.

Tags