Aug 14, 2022 07:27 UTC
  • Mafuriko yaua watu zaidi ya 50 nchini Sudan

Makumi ya watu wameaga dunia kufuatia mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini Sudan.

Hayo yalisemwa jana Jumamosi na Brigedia Jenerali Abdul-Jalil Abdul-Rahim, Msemaji wa Baraza la Taifa la Ulinzi wa Raia na kuongeza kuwa, mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Sudan yamesababisha watu 50 kuaga dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza msimu wa mvua nchini humo.

Amesema, mkoa wa Kordofan Kaskazini unaongoza kwa idadi ya vifo vya janga hilo la kimaumbile, ambapo watu 19 wameripotiwa kuaga dunia, huku vifo 16 vikiripotiwa katika eneo la Darfur Magharibi lenye mikoa 5, na watu 7 wakipoteza maisha katika mkoa wa Mto Nile.

Shirika rasmi la habari la Sudan SUNA limemnukuu Brigedia Jenerali Abdul-Rahim akisema kuwa, watu 25 wamejeruhiwa kwenye janga hilo, huku nyumba 8,170 zikisombwa na maji ya mafuriko. Aidha mashamba ya kilimo yenye ukubwa wa ekari 540 yamesombwa pia.

Maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mafuriko

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema watu zaidi ya 38,000 wameathiriwa na mafuriko na athari nyingine za mvua hizo za msimu nchini Sudan, tokea mwezi Mei mwaka huu.  

Mvua kubwa hunyesha nchini Sudan kati ya mwezi wa Mei na Oktoba, na nchi hiyo hukumbwa na mafuriko makubwa kila mwaka ambayo mbali na kuua, huharibu mali, miundombinu na mazao. Mwaka jana janga la mafuriko nchini Sudan liliua watu wengine zaidi ya 80 huku watu 102,000 wakiathiriwa na janga hilo la kimaumbile.

Tags