Aug 15, 2022 02:29 UTC
  • Watu 41 wapoteza maisha kufuatia moto ndani ya Kanisa la Koptik nchini Misri

Watu zaidi ya 41 wamepoteza maisha baada ya moto kuenea ndani ya Kanisa la Koptik katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Taarifa zinasema moto huo umeteketeza sehemu ya Kanisa la Koptik la Abu Sifine katika mtaa wa Imbaba, kaskazini magharibi mwa Cairo.

Wazimamoto walifanikiwa kuuzima moto huo ambao sababu za kuanza kwake bado hazijulikani.

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ametangaza katika ukurasa wake wa Facebook kuwa, ameamuru mashirika yote ya kiserikali kuchukua hatua za kutoa huduma zinazohitajika baada ya maafa hayo.

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri

Rais Sisi, ambaye ni rais wa kwanza wa Misri kuhudhuria Misa ya Krismasi katika Kanisa la Koptik amesema amezungumza kwa simu na kiongozi wa kanisa hilo Misri, Papa Tawadros II na kumpa salamu za rambi rambi.

Kanisa la Koptik nchini Misri limethibitisha kuwa watu 41 wamepoteza maisha na wengine 14 wamejeruhiwa katika tukio hilo. Idara ya Mwendesha Mashtaka Misri imetangaza kuanza uchunguzi.

Wakopti ni idadi kubwa zaidi ya jamii ya Wakristo katika nchi ya Kiarabu ambapo idadi yao ni milioni 10 kati ya watu milioni 103 nchini humo.