Aug 15, 2022 04:14 UTC
  • Mwito wa amani watolewa huku Wakenya wakiendelea kusubiri matokeo ya urais

Viongozi wa kidini na wakuu wa asasi za kiraia wametoa mwito kwa wananchi wa Kenya kuendelea kudumisha amani na kuwa watulivu huku wakisuburi matokeo ya uchaguzi wa rais.

Asasi za kiraia na mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiongozwa na Amnesty International na Transparency International yametoa taarifa ya pamoja yakiwaasa wanasiasa, wagombea wa viti mbalimbali na Wakenya wote kwa ujumla kuwa na utulivu, wakati huu ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapoendelea kujumlisha na kuhakiki matokeo ya kura za rais.

IEBC ina hadi kesho Jumanne kumtangaza mshindi wa urais kwa mujibu wa katiba na sheria za uchaguzi nchini humo. Mchuano mkali umeendelea kuwa kati ya mgombea wa chama cha UDA, William Ruto na Raila Odinga aliyegombea kwa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyohakikiwa na gazeti la The Star na shirika la habari la Reuters mpaka sasa, Ruto ambaye ni Naibu Rais anaongoza kwa kura milioni 7.1, huku Odinga ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu akipata milioni 6.9. Hayo ni kwa mujibu wa matokeo yaliyohakikiwa ya maeneobunge 272 kati ya 290.

Ruto (kulia) na Odinga

Wachambuzi wa kisiasa wanasema, uwezekano wa mgombea wa kiti cha rais atakayeshindwa kwenda katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ni mkubwa, na hivyo huenda Wakenya wakalazimika kusubiri zaidi kumjua rais mpya atakayerithi mikoba ya Uhuru Kenyatta.

Mshindi wa urais sharti apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa, na asilimia 25 ya kura katika angalau kaunti 24 kati ya 47 za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Tags