Aug 15, 2022 15:43 UTC
  • William Ruto atangazwa mshindi wa kinyang'ayiro cha urais nchini Kenya

William Ruto mgombea wa Urais kupitia Chama cha UDA nchini Kenya ametangazwa kuwa mshindi wa kinyang'anyiro hicho na sasa ndiye Rais mteule wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

William Ruto ameibuka mshindi baada ya kumpiku mpinzani wake mkuu na wa karibu Raila Amollo Odinga wa Muungano wa Azimio.

Akitangaza matokeo hayo leo katika ukumbi wa Bomas, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya Wafula Chebukati amesema kwamba, Ruto amejipatia asilimia 50.49 ya kura huku Odinga akishika nafasi ya pili baada ya kujipatia asilimia 48.85 ya kura.

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya IEBC imemtangaza Naibu Rais William Ruto kuwa rais mteule, kufuatia uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali, akimshinda mwanasiasa wa muda mrefu na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Raila Odinga ameshindwa na William Ruto katika mbio za kuwania urais nchini Kenya

 

Ruto ametangazwa mshindi huku kukiwa na mgawanyiko baada ya mgombea wa Muungano wa Azimio Raila Odinga kususia sherehe ya kumtangaza mshindi.

Hata hivyo zoezi hilo limekumbwa na wimbi la utata baada ya makamishna wanne wa tume ya IEBC kutangaza kutotambua matokeo ya uchaguzi wa rais wakidai kuwa, mchakato huo umekosa uwazi katika hatua za mwisho.

Kwa matokeo hayo, William Ruto atamrithi Rais Uhuru Kenyatta anayemaliza muda wake na hivyo kuwa Rais wa tano wa taifa la Kenya.