Aug 16, 2022 03:40 UTC
  • Wakenya wasubiri muelekeo wa Odinga baada ya Ruto kutangazwa mshindi wa urais

Wananchi wa Kenya hususan wafuasi wa mwanasiasa mkongwe Raila Odinga wanasubiri tangazo na muelekeo utakaochukuliwa na mgombea huyo wa kiti cha rais kupitia chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya katika uchaguzi wa Jumanne iliyopita, baada ya mshindani wake William Ruto wa chama cha UDA kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo.

Dalili zote zinaashiria kuwa Odinga, ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya ataelekea mahakamani kupinga matokeo hayo. Mahakama ya Juu ndiyo yenye wajibu wa kisheria wa kusikiliza shauri la kupinga matokeo ya urais.

Mawakala wakuu wa chama cha Odinga katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, hiyo jana walisema kuwa hawakuridhishwa na mchakato wa kujumlisha na kuhakiki matokeo ya kura za urais. Wanasisitiza kuwa mchakato huo haukuwa na uwazi na uligubikwa na mizingwe, mbali na kudukuliwa mfumo wa kuhifadhi matokeo hayo. 

Macho yote sasa yataelekezwa katika Mahakama Juu chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu, Martha Koome, korti ambayo mwaka 2017 chini ya David Maraga ibatilisha pia matokeo ya urais.

Jana Jumatatu, William Ruto mgombea wa urais kupitia chama cha UDA nchini Kenya alitangazwa kuwa mshindi wa kinyang'anyiro hicho na sasa ndiye Rais mteule wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) Wafula Chebukati alisema kwamba, Ruto amejipatia asilimia 50.49 ya kura huku Raila Odinga aliyewania kwa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya akishika nafasi ya pili baada ya kujipatia asilimia 48.85 ya kura.

Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) anayeondoka madarakani na Rais mteule, William Ruto

Hata hivyo zoezi hilo limekumbwa na wimbi la utata baada ya makamishna wanne wa tume ya IEBC kutangaza kutotambua matokeo ya uchaguzi wa rais wakidai kuwa, mchakato huo umekosa uwazi katika hatua za mwisho.

Katika hali ambayo Wakenya katika ngome za kisiasa za Ruto hususan mkoa wa Bonde la Ufa na baadhi ya maeneo ya Mlima Kenya wamesherehekea usiku kucha ushindi huo, fujo za hapa na pale zimeshuhudiwa katika ngome za Odinga, kama vile mtaa wa Kibra jijini Nairobi na jijini Kisumu, huku akthari ya watu wakijifungia majumbani katika baadhi ya miji kama Mombasa.

Tags