Aug 16, 2022 08:04 UTC
  • Marais, viongozi wa kieneo wampongeza Rais mteule wa Kenya, William Ruto

Marais a viongozi wa nchi kadhaa za Afrika wamemnyooshea mkono wa pongezi William Ruto kwa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa kiti cha rais nchini Kenya uliofanyika wiki iliyopita.

Katika salamu zake za pongezi, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewapongeza wananchi wa Kenya kwa kufanya uchaguzi kwa amani, na kusisitiza kuwa taifa lake linatarajiwa kuendelea kushirikiana na Wakenya kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa nchi mbili hizo za Afrika Mashariki. 

Aidha Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amempongeza Ruto kwa kutangazwa kuwa Rais mteule wa Kenya katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali baina yake na mwanasiasa mkongwe Raila Odinga.

Mnangagwa ameandika katika ujumbe wa Twitter kuwa: Pongezi kwa William Ruto kwa kutangazwa Rais ajaye wa Kenya. Sina shaka kwamba atalitumikia taifa lake na bara letu kwa ufanisi.

Wakati huohuo, Rais wa sasa wa Somalia, Hassan Mohamud na mtangulizi wake Mohammed Farmaajo kwa nyakati tofauti wamempa mkono wa tahani Ruto kwa ushindi huo. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) Wafula Chebukati jana alitangaza kuwa, Ruto amejipatia asilimia 50.49 ya kura, huku Odinga aliyewania kwa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya akishika nafasi ya pili baada ya kujipatia asilimia 48.85 ya kura.

Mama Samia

Kadhalika Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, amempongeza Ruto mwenye umri wa miaka 55 kwa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Kenya uliofanyika Jumanne iliyopita ya Agosti 9. 

Katika ujumbe wake wa pongezi, Ahmed amesema: Nakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yaliyoko mbele yako. Tunatazamia kufanya kazi kwa karibu sana pamoja nawe, juu ya masuala yenye maslahi ya pamoja kieneo na kimataifa.

Odinga (kulia) na Rais anayeondoka, Uhuru Kenyatta

Salamu hizo za pongezi zinaendelea kumiminika huku hali ya taharuki ikitanda katika baadhi ya maeneo, na sasa macho na masikio yameelekezwa kwa Odinga, ambaye anasubiriwa kutoa tangazo na muelekeo atakaochukua. Mwanasiasa huyo (77) ambaye alikuwa anawania urais kwa mara ya tano, anatazamiwa kwenda Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Tags