Aug 16, 2022 12:13 UTC
  • Ukomo wa uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali

Sambamba na kuendelea mvutano kati ya Ufaransa na Mali, hatimaye Paris imetangaza ukomo wa uwepo wa wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Vikosi vya wanajeshi 2,400 wa Ufaransa vimekuwepo nchini Mali kwa takriban miaka 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Mabaki ya wanajeshi wa Ufaransa waliondoka nchini Mali jana Jumatatu, kuashiria mwisho wa Operesheni ya Barkhane katika nchi hiyo ya eneo la Sahel barani Afrika. Taarifa ya Vikosi vya Jeshi la Ufaransa imesema, askari wa mwisho wa kikosi cha Barkhane waliokuwa katika ardhi ya Mali wameondoka na kuvuka mpaka baina ya nchi hiyo na Niger.

Mvutano kati ya Ufaransa na Mali ulipamba moto katika miezi ya hivi karibu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya 2021 katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, wakati Kanali Assimi Goïta alipotwaa madaraka ya nchi. Maafisa wa serikali ya Mali wanawatuhumu wanajeshi wa Ufaransa kuwa, wanashirikiana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kufanya ukatili dhidi ya raia na kushindwa kukabiliana ipasavyo na makundi ya kigaidi.

Baada ya Baraza la Kijeshi la Mali kuanza kazi lilitangaza kuwa haliyatambui makubaliano ya ulinzi baina ya nchi hiyo na Ufaransa na kwamba halitayatekeleza. Serikali ya Mali pia ilimfukuza balozi wa Ufaransa mjini Bamako, kitendo ambacho kilikabiliwa na hisia kali ya serikali ya Paris. Kwa msingi huo, uhusiano wa Bamako na Paris ukawa umeingia katika anga na mazingira mapya.

Wanachama wa moja ya makundi ya waasi nchini Mali

 

Wataalamu wa mambo wamekuwa wakitilia shaka madai ya Ufaransa ya kuweko jeshi lake nchini Mali kwamba, ni kwa ajili ya kupambana na makuundi ya kigaidi. Tathmini mbalimbali zinaonyesha kuwa, katika miaka hii yote ya kuweko wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel Afrika yameshadidisha harakati zao sambamba na kukithirisha hujuma na mashambulio yao ya kigaidi hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Hujuma hizo zimesababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Choguel Kokalla Maiga, Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Mali amewahi kunukuliwa akisema kuwa: Kuna ushahidi unaoonyesha kuwa, wanajeshi wa Ufaransa anmbao walikuja katika ardhi yetu kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi, wamekuwa wakitoa mafunzo kwa makundi hayo na magaidii hao wamefanikiwa kudhibiti theluthi mbili ya ardhi ya nchi.

Filihali, Ufaransa imelazimika kuondoa wanajeshi wake baada ya viongozi wa Mali kung'ang'ania msimamo wa kuondolewa majeshi hayo. Pamoja na hayo, viongozi wa Ufaransa wametangaza kuwa, wanahamishia askari wao hao katika moja ya nchi za Sahel Afrika.

Hii inaonyesha kuwa, licha ya Ufaransa kulazimika kuondoa askari wake nchini Mali kufuatia mashinikizo ya viongozi wa Bamako, lakini kimsingi haiko tayari kuondoka kikamilifu barani Afrika. Hili ni moja ya mambo yanayoshadidisha ushindani baina ya madola makubwa huko barani Afrika.

Assimi Goita, kiongozi wa Malii

 

Pamoja na kuwa, mataifa ya Afrika daima yamekuwa kitovu cha ushindani na kupimana misuli wakoloni kutokana na kuwa na maliasili na vyanzo vya utajiri, lakini ushindani huo umeshika kasi zaidi baada ya kutokea mabadiliko katika siasa za kimataifa hususan baaada ya kuzuka vita baina ya Ukraine na Russia.

Wataalamu wa matukio ya Afrika wanasema kuwa, mataifa ya Magharibi yamekuwa yakifuatilia maslahii yao yale yale ya huko nyuma kama vile kuimarisha zaidi uwepo wao barani humo, kupora vyanzo vya utajiri vya Waafrika, kuyatwisha mataifa ya Kiafrika mipango yao ya kujidhaminia fedha na kuchochea sambamba na kuanzisha migogoro ya kijeshi lengo likiwa ni kuziuzia silaha pande zote zinazozozana.

Hii ni katika hali ambayo mkabala wa hilo, kiwango cha utambuzi kwa fikra za waliowengi, moyo wa kupigania mamlaka ya kujitawala na kuchukia ukoloni vimeongezeka mno miongoni mwa mataifa ya Kiafrika na akthari ya mataifa hayo hayavumilii hata kidogo kuendelea kuweko askari ajinabi katika nchi zao.

Kuhusiana na hilo, William Gumede, Mkurugenzi wa Democracy Works Foundation anasema: Inaonekana kuwa, vita vipya vya baridi vimo mbioni kutokea barani Afrika.

Hali hii katika hatua ya awali bila shaka itashadidisha matatizo yanayoyakabili mataifa ya Afrika.

Tags