Aug 16, 2022 13:56 UTC
  • Magaidi wa Al Qaida Mali wadai kuua washauri wa kijeshi wa Russia

Magaidi wanaofungamana na kundi Al Qaeda nchini Mali Jumatatu wamedai kuwaua washauri wanne wa kijeshi wa Shirika la Huduma za usalama la Wagner la Russia katika shambulio la kuvizia karibu na eneo la Bundiagara katikati mwa Mali.

Kitengo cha habari cha kundi la kigaidi la NIM linalofungamana na Al Qaeda, kimesema katika taarifa kwamba wapiganaji wa kundi hilo walipambana na washauri hao wa kijeshi wa  Shirika la Wagner  Jumamosi katika jimbo la Mopti. Wagner haina mwakilishi wa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari na haikuweza kupatikana ili kutoa maelezo.

Mali iko mbioni kukabiliana na magaidi wakufurishaji wanaopata himaya ya kigeni  ambao walianzisha ghasia zao mwaka 2012 na kuenea tangu wakati huo katika nchi jirani, na kuua maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuhama makazi yao katika eneo la Sahel la Afrika magharibi.

Wagner ilianza kupeleka mamia ya washauri wake wa kijeshi mwaka jana kulisaidia jeshi la Mali baada ya askari wa kigeni wakiongozwa na Ufaransa kushindwa kukabiliana na magaidi hata baada ya kuwako katika nchi hiyo kwa muda wa miaka 10. Hayo yanajiri baada ya mabaki ya wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini Mali jana Jumatatu, kuashiria mwisho wa Operesheni ya Barkhane katika nchi hiyo ya eneo la Sahel barani Afrika.

Askari wa Jeshi la Mali

Taarifa ya Vikosi vya Jeshi la Ufaransa imesema, askari wa mwisho wa kikosi cha Barkhane waliokuwa katika ardhi ya Mali wameondoka na kuvuka mpaka baina ya nchi hiyo na Niger. 

Maafisa wa serikali ya Mali wanawatuhumu wanajeshi wa Ufaransa kuwa wanashirikiana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kufanya ukatili dhidi ya raia na kushindwa kukabiliana ipasavyo na makundi ya kigaidi.