Aug 16, 2022 14:27 UTC
  • Mgombea urais wa Azimio Kenya apinga matokeo yaliyomtangaza Ruto mshindi

Raila Odinga, mgombea urais wa Kenya kwa tiketi ya Muungano wa Azimio amesema hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC kwa sababu mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alikiuka katiba kabla ya kumtangaza mshindi.

Akizungumza na vyombo vya habari leo jioni katika mji mkuu Nairobi, Odinga ameeleza kwamba, makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliyompatia ushindi mshindani wake mkuu William Ruto.

"Takwimu zilizotangazwa na Chebukati ni batili kwa maoni yetu, hakuna mshindi kisheria aliyetangazwa kihalali wala rais mteule", amesisitiza Odinga.

Hata hivyo Raila Odinga amewataka wafuasi wake kudumisha amani na utulivu huku muungano wake ukifuata njia za kikatiba za kubatilisha matamshi ya Chebukati.

Amefafanua kwa kusema: "jana, demokrasia yetu changa ilikumbwa na msukosuko mkubwa, kwa sababu hiyo, Kenya inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisheria na kisiasa kutokana na matendo ya Wafula Chebukati".

Wafula Chebukati

 

Mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya muungano wa Azimio ameongezea kwa kusema: "tunafuatilia njia za kisheria na za amani. Tuna hakika kwamba haki itatendeka. Tunaelewa kuwa ni Bwana Chebukati pekee ndiye aliyepata kujumlisha kura za urais. Aliwanyima makamishna wote kupata taarifa hizo".

Matamshi ya Odinga yamejiri muda si mrefu baada ya makamishna wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi kujitenga na matokeo, wakidai kwamba yalikumbwa na 'kiza kinene'.

Makamishna hao wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera wamesema, hawakukubaliana kuhusu matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati.

Wamesema hesabu iliyotolewa na Chebukati ya asilimia 100.1 haikulingana na jumla ya matokeo ya urais ya wagombea wote wanne.

Akizungumza na waandishi wa habari, Raila ameongezea kwamba, mwenyekiti huyo hakujadiliana na makamishna wenzake kuhusu matokeo hayo kabla ya kuyatangaza.../

 

Tags