Aug 17, 2022 12:06 UTC
  • Katiba mpya inayompa rais mamlaka makubwa yaanza kutekelezwa Tunisia

Katiba mpya ya Tunisia inayompa rais wa Jamhuri nguvu na mamlaka mengi na makubwa imeanza kutekelezwa, baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo rasmi ya mwisho ya kura ya maoni iliyofanyika mwezi uliopita.

Katiba hiyo mpya inaanza kutekelezwa rasmi katika nchi hiyo ya ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika baada ya matokeo hayo kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali.

Kwa mujibu wa matokeo hayo rasmi, asilimia 96 ya washiriki wa kura ya maoni walipiga kura ya 'Ndio' ya kuunga mkono rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Rais Saied. Bodi hiyo ya uchaguzi nchini humo, hata hivyo, imesema waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 31 pekee ya wapiga kura waliostahili.

Asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya serikali nchini Tunisia yametilia shaka uhalali wa matokeo ya kura hiyo ya maoni ya kubadilisha katiba.

Kupasishwa kwa katiba mpya nchini Tunisia kunamaanisha kuwa, Rais Kais Saied ataruhusiwa kuwasilisha miswada ya sheria na kuwa na mamlaka makubwa ya kupendekeza mikataba mbalimbali, mbali na kuandaa bajeti za serikali.  

Maandamano ya Watunisia ya kupinga katiba mpya

Hii ni katika hali ambayo, mashirika ya kiraia na vyama vya kisiasa nchini humo vinamtaka Rais Kais Saied kuachia ngazi na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mapema nchini humo.

Tunisia iko kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa tangu Julai 25 mwaka jana 2021, wakati Saied alipoivunja serikali, kusimamisha bunge na kutwaa mamlaka yote ya nchi.

Tags