Aug 18, 2022 07:29 UTC
  • Mali yasema Ufaransa inasaidia magaidi, yaitisha kikao Baraza la Usalama

Mali imeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya mkutano wa dharura ili kusitisha kile inachokitaja kuwa ni "vitendo vya uchokozi" vinavyofanywa na Ufaransa kwa kukiuka mamlaka yake, kuunga mkono makundi ya magaidi wakufurishaji na ujasusi.

Barua iliwasilishwa kwa waandishi wa habari na Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali siku ya Jumatano baada ya kukabidhiwa balozi wa China katika Umoja wa Mataifa ambaye ni mwenyekiti wa mzunguko wa  Baraza la Usalama.

Katika barua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop amesema nchi yake "inahifadhi haki ya kujilinda" ikiwa hatua za Ufaransa zitaendelea, kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Barua hiyo iliandikwa tarehe 15 Agosti, tarehe ya kuondoka kwa mwanajeshi wa mwisho wa Ufaransa nchini Mali baada ya miaka tisa ya makabiliano yaliyofeli na makundi ya kigaidi.

Viongozi wa kijeshi walio madarakani nchini Mali tangu mwezi Agosti 2020 wameamua kusitisha ushirikiano na  Ufaransa na sasa wanashirikiana na Russia katika vita dhidi ya magaidi.

Katika barua hiyo, Diop amelaani "ukiukaji wa mara kwa mara" wa anga ya taifa la Mali unaofanywa na vikosi vya Ufaransa na safari za ndege za Ufaransa zinazohusika na "shughuli zinazochukuliwa kuwa za kijasusi" na majaribio ya "kutisha".

Ameongeza kuwa  Mali ina "ushahidi kwamba ukiukwaji huu wa wazi wa anga ya Mali ulitumiwa na Ufaransa kukusanya taarifa za kijasusi kwa vikundi vya kigaidi vinavyoendesha shughuli zao katika Sahel na kuwafikishia silaha magaidi hao."

Ufaransa hadi sasa imejizuia kujibu kauli hiyo ya serikali ya Mali.

Vikosi vya wanajeshi 2,400 wa Ufaransa vimekuwepo nchini Mali kwa takriban miaka 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Mabaki ya wanajeshi wa Ufaransa waliondoka nchini Mali Jumatatu, kuashiria mwisho wa Operesheni ya Barkhane katika nchi hiyo ya eneo la Sahel barani Afrika. 

Mvutano kati ya Ufaransa na Mali ulipamba moto katika miezi ya hivi karibu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya 2021 katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, wakati Kanali Assimi Goïta alipotwaa madaraka ya nchi. 

Tags