Aug 18, 2022 10:28 UTC
  • Idadi ya ya waliopoteza maisha katika moto wa msituni Algeria yaongezeka

Idadi ya waliopoteza maisha katika moto wa msituni nchini Algeria imeongezeka na kufikia wahanga 36.

Awali iliripotiwa kuwa watu 26 wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa katika moto wa msituni katika wilaya 14 za kaskazini mwa Algeria.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Algeria Kamel Beldjoud ameiambia televisheni ya taifa kwamba watu 24 wamepoteza maisha katika moto huo katika eneo la  El Tarf, karibu na mpaka na Tunisia, pamoja na wengine wawili waliokufa mapema Jumatano huko Setif.

Leo duru za habari zimeripoti kuwa, idadi ya vifo imeongezeka na kufikia watu 36.

Idara ya ulinzi wa raia huko Setif imesema wanawake wawili, mama mwenye umri wa miaka 58 na binti yake mwenye umri wa miaka 31”, walifariki katika mji huo wa Setif.

 

Katika wilaya ya Souk Ahras, mbali zaidi upande wa mashariki karibu na mpaka wa Algeria na Tunisia, watu walionekana wakikimbia makazi yao huku moto ukitanda kabla ya helikopta za kuzima moto kupelekwa huko.

Ripoti ya awali ilisema watu wanne waliungua huko Souk Ahras na wengine 41 walikuwa na matatizo ya kupumua, maafisa wamesema. Ripoti za vyombo vya habari zimesema wakazi 350 walihamishwa.

Tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti, mioto 106 ilizuka nchini Algeria, ikiharibu zaidi ya hekta 2,500 za misitu.

Kaskazini mwa Algeria huathiriwa na mioto ya misitu kila mwaka, huku watu 90 wakikadiriwa kufariki mwaka jana - na zaidi ya hekta 100,000 za misitu ziliteketezwa.