Aug 18, 2022 10:29 UTC
  • Watawala wa kijeshi Chad wapiga marufuku maandamano ya wapinzani

Viongozi wa kijeshi nchini Chad wamepiga marufuku maandamano ya upinzani yaliyopangwa baadaye wiki hii, kwa madai ya kuchelewa kuwasilisha maombi kwa wakati.

Hiyo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na watawala hao hapo jana. Ripoti zinaeleza kuwa, muungano wa vyama vya upinzani pamoja na asasi za kiraia, wa Wakit Tamma ulikuwa umeitisha maandamano Ijumaa dhidi ya baraza la kijeshi la mpito linalotawala, na linaloongozwa na generali Mahamat Idriss Deby, mwana wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Idriss Deby.

Inaelezwa kuwa, lengo la muungano huo lilikuwa kuanza maandamano siku moja kabla ya kuanza kwa kile kilichotajwa kuwa mjadala wa kitaifa siku ya Jumamosi, kwa lengo la kupanga mikakati kuelekea kwenye uchaguzi mkuu na kurejesha utawala wa kiraia.

Kundi la Wakit Tamma limekataa kushiriki kwenye mazungumzo hayo ambayo yanawaleta pamoja maafisa wa serikali, vyama vya wafanyakazi, upinzani pamoja na asasi za kiraia.

Zoezi la utilianaji saini baina ya wawakilishi wa serikali ya Chad na makundi ya upinzani

 

Muungano huo kupitia taarifa ya pamoja umesema kwamba baraza la kijeshi limepanga kuitisha mazungumzo yanayoegemea upande mmoja kwa kuvitenga vyama vya upinzani vyenye nguvu pamoja na mashirika mengine ya kiraia.

Wiki chache zilizopita, serikali ya kijeshi ya Chad na makundi zaidi ya 40 ya upinzani walisaini makubaliano ya amani mjini Doha, Qatar kwa lengo la kuanzisha mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa, huku kundi kuu la waasi katika nchi hiyo Afrika ya Kati likikataa kusaini mapatano hayo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mazungumzo hayo ya maridhiano ya kitaifa yalipangwa kuanza rasmi tarehe 20 Agosti katika mji mkuu wa Chad N’Djamena ili kufungua njia ya kuitishwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.