Aug 19, 2022 12:08 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Chad arejea nchini baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka 17

Kiongozi wa waasi wa Union of Resistance Forces, UFR amerejea katika mjii mkuu Chad Ndjamena baada ya kuishi uhamishoni nje ya nchi kwa miaka 17.

Timan Erdimi ambaye amerejea nyumbani Alkhamis ni mpwa wa rais wa zamani Idriss Déby Itno. Erdimi aliongoza safu ya waasi ambayo ilishuka kwenye mji mkuu mnamo mwaka 2019 lakini ilizuiliwa na mabomu 2,000 yaliyorushwa na jeshi la Ufaransa. 

Kiongozi huyu wa UFR ni miongoni mwa viongozi wa makundi ya waasi waliosaini makubaliano ya Doha nchini Qatar.

Timan Erdimi alishuka kwenye ndege iliyomrudisha Ndjamena mapema jana akiweka kitanga cha mkono wake wa kulia kifuani. Timan Erdimi amepokelewa kwenye uwanja wa ndege na watu ishirini kutoka familia yake licha ya mvua nyingi iliyokuwa ikinyesha.

Akiongea mara baada ya kuwasili nchini, Erdimi alisema ana furaha kubwa kuona anarejea nyumbani baada ya miaka 17 akiwa uhamishoni, akimuona binti yake, wajukuu zake na jamaa zake.

Idriss Deby

 

 Ameendelea kueleza kuwa sasa ni muhimu kushiriki katika ujenzi wa Chad na aksisitiza kwamba atashiriki katika mazungumzo ya kitaifa yatakayoanza kesho Jumamosi mjini Ndjamena ambayo amesema ndio njia ya mchakato wa uchaguzi "huru na wa kidemokrasia".

Kiongozi huyo wa upionzani alikimbilia uhamishoni baada ya kujaribu kumpindua Idriss Déby Itno. 

Siku ya Jumanne usiku waasi wengine waliokuwa uhamishoni, akiwemo Gassim Cherif, kiongozi wa kundi lililojitenga na CCMSR, kundi jingine muhimu lenye silaha nchini Chad, walirejea nchini humo.../