Aug 20, 2022 03:47 UTC
  • Askari  wa Umoja wa Mataifa DR Congo waondoka mjini Butembo

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) umeondoka katika mojawapo ya miji mikubwa ya mashariki mwa nchi hiyo baada ya maandamano mabaya ya kupinga kushindwa kwake kuwalinda raia, maafisa wa Kongo na Umoja wa Mataifa walisema Alhamisi.

Mji wa Butembo, ambao ni kitovu cha biashara cha takriban watu milioni moja, umekuwa moja ya vitovu vya maandamano ya ghasia dhidi ya MONUSCO tangu mwezi uliopita ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa, wakiwemo raia, walinda amani na polisi wa Kongo.

Jenerali Constant Ndima, gavana wa kijeshi wa jimbo la Kivu Kaskazini, amewaambia waandishi wa habari kwamba mamia ya wanajeshi wa MONUSCO na wafanyakazi wa kiraia huko Butembo wameondoka na kwamba mipango inafanywa kuhusu jinsi ya kuhamisha vifaa vyao.

Ndeye Khady Lo, msemaji wa MONUSCO, hata hivyo amesema kuondoka huko ni kwa muda tu.

Kulingana na msemaji huyo wa muda, MONUSCO itahamisha tu baadhi ya vifaa na wafanyakazi wake kutoka Butembo hadi maeneo mengine nchini, hasa Beni.

“Hatuondoki Butembo. Badala yake tunapeleka baadhi ya nyenzo zetu sehemu nyingine. Bado tunaunga mkono jeshi la DR Congo, FARDC, Butembo na kwingineko Kivu Kaskazini,” Ndeye Khady Lo amesema.

Hivi majuzi, maandamano ya kuipinga MONUSCO yaliyoanza Julai 25, 2022, huko Butembo, yalisababisha vifo vya takriban watu 17. Wananchi wa DRC wanalalamika kuwa licha ya kuwepo zaidi ya askari 16,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo, waasi wanaendelea kuimarika na kutekeleza mauaji dhidi ya raia.