Aug 20, 2022 04:06 UTC
  • Mzozo kuhusu maziko ya dos Santos, rais wa zamani wa Angola

Binti wa rais wa zamani wa Angola Jose Eduardo dos Santos amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Uhispania ulioamuru mwili wake uachiliwe kwa mjane wake na kurudishwa Angola kwa mazishi.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani Alhamisi na Tchize dos Santos, bintiye mwendazake mwenye umri wa miaka 44.

Rais huyo wa zamani ambaye alitawala taifa hilo la Afrika lenye utajiri wa mafuta kwa mkono wa chuma kuanzia 1979 hadi 2017, alifariki dunia mjini Barcelona Julai 8 akiwa na umri wa miaka 79 baada ya kupata mshtuko wa moyo.

Tangu wakati huo, swali la lini na wapi atazikwa limeigombanisha serikali ya Angola na mjane wake, Ana Paula na baadhi ya watoto wake watu wazima.

Siku ya Jumanne, mahakama ya Barcelona iliamuru mabaki yake yapewe Ana Paula na ikatoa idhini ya kurejeshwa mwili Angola".

Lakini binti yake alikata rufaa, akisema mahakama haikuwa na mamlaka ya kutoa uamuzi kuhusu kesi hiyo.

Rufaa hiyo pia inadai kwamba dos Santos na Ana Paula walitengana tangu 2017 na "hawakuishi katika hali ya kawaida ya ndoa".

Tchize dos Santos amesema mara kwa mara babake alitaka kuzikwa huko Barcelona ambako alikuwa akiishi zaidi tangu ajiuzulu mwaka 2017.

Rais Joao Lourenco wa Angola

Pia anadai kuwa mazishi ya babake nchini Angola yanaweza kutumika kupendelea serikali ya sasa ya Joao Lourenco kabla ya uchaguzi mkuu mnamo Agosti 24.

Siku chache baada ya kifo chake, uchunguzi wa maiti ulifanyika kwa ombi lake kwa msingi kwamba alikufa katika "mazingira ya kutia shaka".

Katikati ya Julai, mahakama ya Uhispania ilikataa kuachilia mwili wake hadi vipimo vikamilike. Hatimaye uchunguzi wa maiti ulionyesha kilikuwa kifo cha kawaida.

Wakati wa utawala wa dos Santos ambao ulidumu kwa takriban miaka 40, wanafamilia wake walitumia utajiri wa mafuta wa taifa hilo kujitajirisha huku Waangola wengi wakisalia katika umaskini.

Alipojiuzulu mnamo 2017, dos Santos alimkabidhi madaraka Lourenco, waziri wa zamani wa ulinzi.

Lakini Lourenco alimgeukia haraka na kuanzisha harakati ya kupambana na ufisadi ili kurejesha mabilioni ambayo alishuku kuwa yalikuwa yamevujwa chini ya dos Santos, kampeni ambayo imelenga familia ya rais huyo wa zamani.