Aug 22, 2022 04:24 UTC
  • Waliouawa katika shambulio dhidi ya hoteli Mogadishu wapindukia 20

Watu wasiopungua 21 wameuawa huku wengine 117 wakijeruhiwa, baada ya kundi la kigaidi la la al-Shabaab kuwashika mateka mamia ya watu katika hoteli moja huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Wanachama wa al-Shabaab waliishambulia na kuiteka Hoteli ya Hayat tangu siku ya Ijumaa, lakini mapema jana askari wa Somalia walifanikiwa kuhitimisha shambulio hilo.

Kamanda Mkuu wa Polisi, Meja Abdi Hassan Mohamed Hijar amesema magaidi hao walikuwa wanawatumia mateka kama ngao ya binadamu, jambo ambalo lilitatiza jitihada za maafisa usalama za kukabiliana na mzingiro huo.

Amesema: Vikosi vya usalama vimehitimisha utekaji huo, na wabeba bunduki wote wameuawa. Hata hivyo hajasema idadi ya magaidi, raia au maafisa usalama waliouawa kwenye shambulio hilo.

Idadi kubwa ya raia hasa watoto wadogo na wanawake wameokolewa na maafisa usalama wa Somalia. Hoteli ya Hayat hutumiwa zaidi ya maafisa wa serikali na wanasiasa wa Somalia, hususan Wabunge.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Wakati huohuo, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani hujuma hiyo ya kigaidi iliyopelekea makumi ya watu kuuawa. 

Amesema UN itaendelea kushirikiana na serikali na taifa la Somalia katika mapambano yao dhidi ya ugaidi, na itaendelea kuunga mkono jitihada zao za kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

 

Tags