Aug 28, 2022 13:02 UTC
  • Safari ya Rais wa Ufaransa nchini Algeria

Kufuatia kuendelea mvutano kati ya Ufaransa na Algeria, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameitembelea nchi hiyo ya Kiafrika kwa lengo la kuboresha uhusiano ulioharibika na kufungua "ukurasa mpya" katika uhusiano wa pande mbili.

Safari ya Macron nchini Algeria imefanyika baada ya kuongezeka mvutano wa kisiasa kati ya nchi hizo kutokana na tafsiri na mitazamo tofauti kuhusu vita vya umwagaji damu vya kupigania uhuru wa Algeria. Mwishoni mwa mwaka jana, Algeria ilimwita nyumbani balozi wake kutoka Ufaransa kuhusiana na suala hilo hilo.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Emmanuel Macron aliushutumu "mfumo unaotawala wa kisiasa na kijeshi" wa Algeria kwa kutumia kumbukumbu za vita vya uhuru kuendeleza uhai wake na kuhalalisha uwepo wake. Macron pia alihoji kuwepo kwa "taifa la Algeria kabla ya ukoloni wa Ufaransa" na kusisitiza haja ya kushughulikia suala hilo ili kuleta "maelewano kati ya wananchi".

Sasa, baada ya kupita miezi kadhaa, Macron amesafiri Algeria kwa lengo la kujaribu kurudisha uhusiano wa nchi hizo katika hali ya kawaida.

Rais Emmanuel Macron katika safari yake ya karibuni nchini Algeria

Kwa hakika, safari hiyo ya Macron ni jaribio la kuficha tena jinai za Wafaransa nchini Algeria na kukataa uongozi wa Ufaransa kuomba msamaha kuhusu uhalifu wao wakati wa vita vya uhuru vya Algeria.

Katika kipindi cha kuikoloni Algeria, Ufaransa ilifanya jinai kubwa dhidi ya Waalgeria huku ikipora rasilimali zao, pamoja na kufanya majaribio ya nyuklia katika ardhi ya nchi hiyo kwa madhara ya wakaazi wake. Kwa hivyo, viongozi wa Algeria mara kwa mara wamekuwa wakitaka nchi hiyo kuombwa msamaha rasmi na viongozi wa Paris. Lakini sio tu kwamba viongozi wa Ufaransa wamekataa kuomba msamaha, bali Macron sasa anajaribu kuyataja matukio hayo machungu na ya kuhuzunisha kuwa ni upotoshaji wa historia.

Lengo jingine la safari ya Macron nchini Algeria ni kujadiliana na viongozi wa nchi hiyo kuhusu nishati. Vita kati ya Ukraine na Russia vikiwa vinaendelea huku Ulaya ikikabiliwa na tatizo kubwa la mafuta, Macron anajaribu kurejesha uhusiano kati ya Paris na Algiers ili kupunguza makali ya tatizo hilo. Licha ya kuwa Macron hajazungumzia wazi wazi mahitaji ya nchi yake kuhusu nishati ya gesi wakati wa safari yake huko Algeria, lakini ni wazi kuwa kwa miezi kadhaa sasa, viongozi wa Ulaya wamekuwa wakitafuta njia za kujidhamini gesi kutoka nchi nyingine zinazouza mafuta kwa wingi duniani.

Mashauriano ya kuidhaminia Ufaransa gesi yamekuwa yakifanyika katika hali ambayo Ulaya ina wasiwasi mkubwa juu ya kukabiliwa na uhaba mkubwa wa gesi katika msimu ujao wa baridi kali, jambo ambalo limeashiriwa na Macron mwishoni mwa safari yake kwa kusema: Tuna uhakika juu ya kudhaminiwa Ufaransa nishati katika msimu huu wa baridi kali, na Algeria pia bila shaka itataka kuwa na vyanzo tofauti vya kujidhaminia mapatano yanayotokana na uuzaji wa gesi katika nchi za Ulaya.

"Hosni Ubeidi", Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Ulimwengu wa Kiarabu na Eneo la Mediterania, anasema kuhusiana na suala hili kwamba: Algeria ina nafasi muhimu kwa kuwa na akiba kubwa ya mafuta na gesi na mabomba yanayounganisha nchi hii na Italia pamoja na Uhispania. Hata kama rasilimali ya gesi ya Algeria haiwezi kuziba kabisa pengo lililoachwa wazi na Russia, lakini bila shaka itakuwa na nafasi muhimu katika kukidhi mahitaji ya nishati ya Ulaya kadiri muda unavyosonga mbele.

Jinai za Wafaransa Algeria

Lengo jingine la safari ya Macron nchini Algeria ni kuhusu masuala ya usalama. Kwa kutilia maanani mabadiliko ambayo yametokea katika baadhi ya nchi za Kiafrika, nchi hizo haziko tayari kuvipokea vikosi vya kijeshi vya Ufaransa katika ardhi zao. Kwa hiyo, katika hali ya sasa, Ufaransa ina wasiwasi mkubwa wa kupoteza washirika wake wa zamani barani Afrika na kukabidhi bara hilo tajiri kwa maliasili kwa Russia na China.

Kuhusiana na suala hilo Jaffar Qanadbashi, mtaalamu wa masuala ya Afrika, anasema: Paris ina wasiwasi mkubwa juu ya kupoteza ushawishi wake wa jadi katika bara hilo. Kwa hivyo, kwa kuitembelea Algeria, ambayo ni nchi muhimu ya Kiafrika, Macron anataka kuigeuza nchi hiyo kuwa mfano mzuri wa kukuza uhusiano wake na nchi za Kiafrika na wakati huo huo kurekebisha uhusiano wake ulioharibika na nchi za bara hilo.

Kwa kuzingatia matukio hayo, inaonekana kuwa rais wa Ufaransa anajaribu kuigeuza Algeria kuwa moja ya washirika wakuu wa Paris barani Afrika. Hata hivyo historia ya ukoloni na umwagaji damu ya Wafaransa nchini Algeria ni kikwazo kikubwa cha kufikiwa lengo hilo.

 

Tags