Aug 30, 2022 09:43 UTC
  • Ethiopia: Tuko tayari kufanya mazungumzo kuhusu Bwawa la Renaissance kwa usimamizi wa AU

Ethiopia imesema iko tayarikufanya mazungumzo na Sudan na Misri kuhusu Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) chini ya uangalizi wa Umoja wa Afrika (AU).

 
Balozi wa Ethiopia mjini Khartoum, Sudan Yibeltal Aemero, ameeleza katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Addis Ababa ina hakika masuala yote yanaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na mashauriano.
 
Aemero amebainisha kuwa mjazo wa tatu wa GERD umekamilika bila kusababisha madhara kwa Sudan au athari mbaya na hasi kwa nchi mbili za juu katika Mto Nile, akimaanisha Sudan na Misri.
 
Balozi wa Ethiopia mjini Khartoum amefafanua kuwa zoezi hilo la ujazaji maji limepunguza athari za mafuriko nchini Sudan licha ya madai ya hivi karibuni ya Khartoum kwamba bwawa hilo lingewaathiri vibaya raia milioni 20 wa Sudan.

 

Mnamo Agosti 12, serikali ya Ethiopia ilitangaza kukamilika kwa mafanikio zoezi la mjazo wa tatu wa GERD.
 
Sudan, Misri, na Ethiopia zimekuwa zikijadiliana chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya kiufundi na kisheria yanayohusiana na ujazaji na uendeshaji wa bwawa la Ethiopia la Renaissance.
 
Sudan ilipendekeza usuluhishi wa mgogoro uliopo baina ya nchi hizo tatu kuhusu suala la GERD ufanywe kwa ushirikiano wa pande nne za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani, na Umoja wa Afrika lakini  thiopia imelikataa pendekezo hilo.
 
Ethiopia, ambayo ilianza kujenga Bwawa Kubwa la Renaissance mwaka 2011, inatarajia kuzalisha zaidi ya megawati 6,000 za umeme kutokana na mradi huo, wakati Misri na Sudan, ambazo zote mbili ni nchi za juu katika Bonde la Mto Nile zinazotegemea mto huo kwa mahitaji ya maji safi, zina wasiwasi kuwa bwawa hilo linaweza kuathiri rasilimali zao za maji.../

 

Tags