Aug 31, 2022 11:27 UTC
  • Sudan yamwita balozi wa Ethiopia kulalamikia madai ya Addis Ababa kuhusu silaha za wapiganaji wa Tigray

Wizara ya Masshauri ya Kigeni ya Sudan imemwita katika makao makuu ya wizara hiyo balozi wa Ethiopia mjini Kharton na kumkabidhi malalamiko dhidi ya madai ya serikali ya Addis Ababa ya kupita katika anga ya Sudan ndege iliyokuwa imebeba silaha kwa ajili ya kuwapelekea wapiganaji wa jimbo la Tigray.

Ethiopia ilidai hivi karibuni kwamba, imetungua ndege ya kijeshi iliyokuwa imebeba silaha zilizokuwa zikipekewa wapiganaji wa jimbo la Tigray.

Taarifa hiyo ya Ethiopia ilieleza pia kwamba, ndege hiyo ya kivita ilipita katika anga ya Sudan. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imeeleza katika taarifa yake kwamba, inakanusha vikali madai hayo na kwamba, imekabidhi rasmi malalamiko yake kwa balozi wa Ethiopia mjini Khartoum.

Majuzi pia duru moja ya kijeshi ya Sudan ilikanusha vikali madai ya viongozi wa Ethiopia kwamba, ndege ya kivita iliyokuwa imebeba silaha kwa ajili ya wapiganaji wa Tigray ilipita katika anga ya Sudan.

Yilbeltal Aemero Alemu, balozi wa Ethiopia nchini Sudan

 

Afisa mmoja wa jeshi la sudan ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa, madai hayo ya Ethiopia ni ya ajabu, ya upotoshaji na yasiyo na msingi wowote.

Huku hayo yakiripotiwa, serikali ya Ethiopia na wapinagaji wa TPLF wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia kila mmoja ameendelea kumtuhumu mwenzake kwamba, anakwamisha juhudi za upatanishi baina ya pande mbili.

Tangu mwezi Novemba mwaka juzi (2020) jimbo la Tigray limekumbwa na hitilafu na mivutano ya kisiasa kati ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na viongozi wa eneo hilo ambao wakati fulani waliongoza serikali ya Ethiopia.

Vita vinavyoshuhudiwa katika eneo hilo hadi sasa vimesababisha kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.

Tags