Sep 08, 2022 10:37 UTC
  • Upinzani Tunisia kutoshiriki uchaguzi kwa sheria zilizoandikwa na 'rais peke yake'

Muungano mkuu wa upinzani nchini Tunisia umesema wanachama wake, kikiwemo chama cha Kiislamu chenye ushawishi mkubwa cha Ennahdha utasusia uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika mwezi Desemba kuchukua nafasi ya bunge lililovunjwa na Rais Kais Saied wa nchi hiyo.

Uchaguzi huo wa bunge la Tunisia umepangwa kufanyika baada ya kupita takriban mwaka mmoja na nusu tangu rais Saied alipolisimamisha bunge lililokuwa na wabunge wengi wa Ennahdha sambamba na kuvunja serikali, na baadaye kupitisha katiba inayoupa nguvu utawala wake wa mtu mmoja.
Ahmed Nejib Chebbi, mkuu wa Vuguvugu la Uwokovu wa Kitaifa linaloundwa na vyama vya siasa na makundi yanayompinga Kais Saeid amesema, muungano huo umeshaamua rasmi kususia uchaguzi ujao.
Chebbi amesisitiza kuwa, hatua hiyo ni jibu kwa sheria ya uchaguzi iliyoandikwa "na Saied peke yake", ikiwa ni sehemu ya "mapinduzi aliyofanya dhidi ya uhalali wa kikatiba".
Rais Kais Saeid

Hatua ya rais Kais Saied ya kunyakua madraka ya nchi ilikaribishwa na Watunisia waliokuwa wamechoshwa na kile walichokiona kama mfumo mbovu na wa kimirengo ulioanzishwa baada ya mapinduzi ya 2011.

Lakini makundi ya upinzani yanasema, hatua alizochukua kiongozi huyo, zilizofikia kilele kwa katiba mpya iliyopitishwa kwa kura ya maoni mnamo mwezi Julai, na ambayo ilisusiwa na akthari ya Watunisia, ni sawa na kurejea kwenye utawala wa kiimla, katika nchi pekee yenye demokrasia iliyotokana na vuguvugu la Machipuo ya Kiarabu ya mwaka 2011.../

Tags