Sep 11, 2022 11:58 UTC
  • Jeshi la Nigeria laua magaidi 420 wa Boko Haram, ISIS huko Borno

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuwaangamiza mamia ya wanachama wa kundi la kigadi la Boko Haram na lile la ISIS Wilaya ya Afrika Magharibi (ISWAP) kaskazini mwa nchi.

Meja Jenerali Christopher Musa, Kamanda wa Kikosi cha Pamoja cha Kupambana na Ugaidi Kaskazini Mashariki mwa Nigeria amesema magaidi wasiopungua 420 wameuawa katika operesheni zilizofanyika mwezi Agosti katika jimbo la Borno. 

Musa amesema baadhi ya magaidi hao wameuawa licha ya kutorokea katika vichaka na misitu ya karibu, baada ya ngome zao kusambaratishwa.

Meja Jenerali Musa ameongeza kuwa, operesheni hizo za kutokomeza ugaidi katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria zimehusisha wanajeshi wa nchi kavu pamoja na wa angani.

Operesheni dhidi ya magaidi Nigeria

Katika miezi ya karibuni, maelfu ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram na wenzao wa ISWAP wamekuwa wakijisalimisha kwa maafisa usalama huko kaskazini mwa Nigeria.

Magaidi hao wakufurishaji wamekuwa wakitekeleza jinai kaskazini mwa Nigeria na nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon na kupelekea makumi ya maelefu ya watu wasio na hatia kuuawa katika kipindi cha miaka 13 iliyopita, huku mamilioni ya wengine wakiachwa bila makao.

Tags