Sep 13, 2022 08:14 UTC
  • Sudan yachapisha rasimu ya katiba mpya

Serikali ya ya Sudan imechapisha rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo kwa lengo la kuunda mfumo wa kidemokrasia wa mpito ili kukomesha mgogoro uliopo nchini humo.

Wanasheria wa Sudan waliwasilisha nakala ya rasimu hiyo kwa tume ya pande tatu za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na shirika la IGAD. Rasimu hiyo ni  muhtasari wa kazi ya kikundi kazi cha kamati ya wanasheria wa Sudan kwa kushirikiana naa makundi ya kiraia na wanadiplomasia.

Rasimu hiyo imesisitiza udharura wa kuundwa serikali ya kiraia na kutoa mapendekezo ya kuanzishwa Baraza Kuu la Jeshi na Baraza la Ulinzi na Usalama linaloongozwa na makundi ya kiraia, baraza la utawala wa kiraia na baraza la mawaziri lenye mamlaka ya kitaifa.

Rasimu ya katiba mpya ya Sudan pia inapendekeza kunganishwa vikosi vya radiamali ya haraka na harakati za wapiganaji wenye silaha katika jeshi la Sudan, na vilevile jeshi lisijihusishe na shughuli za kibiashara na uwekezaji.

Rasimu ya katiba mpya ya Sudan inakuja wakati mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Volker Peretz akiwa na wasiwasi wa kupotezwa fursa za kipindi cha mpito cha kidemokrasia na kusambaratika kwa nchi hiyo kufuatia kushindwa kwa juhudi za kufikia muafaka wa kisiasa ili kumaliza mzozo uliopo nchini Sudan.

Sudan ilitumbukia katika machafuko na mgogoro mkubwa tangu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25 yaliyofanywa na mkuu wa jeshi la nchi hiyo, Abdel Fattah al-Barhan.

Wasudani wakifanya maandamano dhidi ya serikali ya kijeshi

Jenerali al-Barhan aliwafutilia mbali raia kutoka kwenye serikali na tangu wakati huo Wasudani wamekuwa wakiandamana dhidi ya serikali ya kijeshi kudai utawala wa kiraia.

Tags