Sep 13, 2022 11:29 UTC
  • William Ruto aapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya

William Samoei Ruto ameapishwa kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF).

Rais William Ruto amekula kiapo cha kulitumikia taifa leo Jumanne katika hafla zilizofanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.

Watu zaidi ya 60,000 wameruhusiwa kuingia katika uwanja huo kushuhudia historia mpya ya uongozi ikiandikwa nchini humo. Shughuli ya kumuapisha Ruto imeongozwa na Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama, Anne Amadi mbele ya Jaji Mkuu ambaye pia ni Rais wa Mahakama ya Juu, Martha Koome.

Dakta Ruto amekabidhiwa zana za uongozi ikiwemo nakala ya Katiba na kitara cha urais (Presidential sword), huku pia Rigathi Gachagua akiapishwa pia kuwa Naibu Rais wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Marais na wakuu wa serikali na nchi mbalimbali hususan wa kieneo wakiwemo Marais Yoweri Museveni wa Uganda, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Paul Kagame wa Rwanda, na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Mohammed miongoni mwa wengine, walihudhuria sherehe hizo.

Uhuru Kenyatta (kushoto) na Raila Odinga

Ruto alimshinda Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika uchaguzi wa Agosti 9 katika kinyang'anyiro cha kumrithi Uhuru Kenyatta, ambaye amemaliza mihula miwili ya uongozi.

Odinga alipinga ushindi wa Ruto katika Mahakama ya Juu ya Kenya, lakini jopo la majaji saba wa mahakama hiyo liliidhinisha matokeo hayo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC.

Ruto anachukua madaraka ya nchi wakati huu ambapo taifa la Kenya linasumbuliwa na matatizo ya kiuchumi na kijamii, yaliyosababishwa pakubwa na janga la Corona na vita vya Ukraine. 

Tags