Sep 22, 2022 09:41 UTC
  • Waafrika Kusini wataka Uingereza irejeshe almasi iliyoporwa iliyo katika fimbo ya Malkia

Wito umeongezeka nchini Afrika Kusini kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza kwa ajili ya kurejeshwa kwa almasi ya kipekee iliyoporwa na wakoloni Waingereza nchini humo.

Raia wa Afrika Kusini wanadai kurejeshwa kwa almasi hiyo ambayo ni maarufu kama 'Nyota Kubwa ya Afrika, ambayo iko pamoja na vito vingine katika Mnara wa London.

Wananchi wa Afrika Kusini wanasema kwamba jiwe hilo la thamani -- almasi kubwa zaidi isiyo na rangi duniani, ambayo imewekwa kwenye fimbo ya kifalme ambayo ilikuwa mali ya Malkia -- ni kito cha kitamaduni ambacho kilikamatwa na wanajeshi wa kikoloni wa Uingereza wakati huo na kuhamishiwa London.

Hata hivyo, almasi na fimbo yake ni kati ya vitu vya thamani zaidi katika Hazina ya Kifalme ya Uingereza na yamkini wakuu wa London watakaidi matakwa ya kurejesha almasi hiyo.

Kwa ukubwa wake na usahihi wa kiufundi, Nyota Kubwa ya Afrika, pia inajulikana kama Cullinan Diamond, na ni ya aina yake duniani.

Jiwe hilo la vito lenye umbo la pea, ambalo lina uzito wa gramu 26.5 na lina pande 74 na uwazi wa ajabu, linadhaniwa kuwa na thamani ya soko ya angalau dola milioni 400.

Wapigania uhuru wa Kenya wakiwa wanashikiliwa katika kambi za ukandamizaji za mkoloni Muingereza

Almasi hiyo iliporwa kutoka Afrika Kusini mwaka 1905 na "ilitunukiwa" Mfalme Edward VII na serikali ya Koloni ya Transvaal ya Uingereza.

Zaidi ya watu 7,000 wametia saini ombi la kurejesha almasi hiyo, kulingana na tovuti ya Change.org.

Raia wengi wa Afrika Kusini hivi majuzi walidhihirisha wazi takwa hilo kwenye mitandao ya kijamii.

Hayo yanajiri wakati ambao hivi karibuni, Chama cha The Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini kilisema hakiombolezi kifo cha Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza aliyefariki Septemba 8.

Taarifa ya EFF ilisema Elizabeth alichukua hatamu za uongozi Uingereza mwaka 1952, na kutawala kwa miaka 70 kama mkuu wa ufalme ambao ulidumishwa na urithi wa kikatili wa kudhalilisha utu wa mamilioni ya watu duniani kote.

Taarifa hiyo ilisema: "Hatuombolezi kifo cha Elizabeth, kwa sababu kwetu kifo chake ni ukumbusho wa kipindi cha kutisha sana Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla."

Taarifa hiyo imekumbusha kuhusu jinai za utawala wa kikoloni wa Uingereza nchini Afrika Kusini ambapo utajiri ulioporwa nchini humo ulitajirisha familia ya kifalme ya Uingereza.