Sep 25, 2022 10:01 UTC
  • Ethiopia: Dunia inakabiliwa na changamoto ambazo ili kuzitatua panahitajika hatua za maana

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ethiopia amesema kuwa, dunia inakabiliwa na mitihani na changamoto nyingi ambazo ili kuzitatua panahitajika kuchukuliwa hatua za maana na madhubuuti.

Demeke Mekonnen Hassen amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, hivi sasa dunia imejikuta ipo njia panda kuanzia suala la mabadiliko ya tabianchi, umasikini uliokithiri, migogoro, ugaidi na mivutano ya kimataifa.

Aiidha ameeleza kuwa, athari za changamoto hizo ni kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya watu na dunia na cha kusikitisha zaidi ni kuwa, “kiwango cha ushirikiano wa kimataifa hivi sasa hakiko katika nafasi inayostahili kushughulikia changamoto hizo.”

Naibu Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia amesema bayana kwamba, ingawa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inaikumba dunia nzima, lakini wanaoathiriwa zaidi ni wale ambao kimsingi hawahusiki katika uzalishaji wa gesi chafu inayochangia tatizo hilo, mfano wa hilo ni eneo la Pembe ya Afrika. 

Ukame ni moja ya changamoto zinayoyakabili baadhi ya maeneo ya dunia hasa Pembe ya Afrika na Sahel Afrika

 

Kuhusu kulifanyia mabadiliko Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waziri huyo wa Ethiopia amesema, wakati umefika sasa wa kuhakikisha chombo hicho muhimu cha Umoja wa Mataifa kinakwenda na wakati na hali halisi ya sasa duniani, kikiwa jumuishi na chenye usawa.

Demeke Mekonnen Hassen amefafanua zaidi kwa kusema, kwa mfano “Afrika haina kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Usalama la Umoja wa Mataifa jambo ni mfano wa wazi wa kutokuweko uadilifu katika chombo hicho, na ndio maana kilio kikubwa cha Waafrika ni kufanyika mabadiliko katika muundo wa chombo hicho.