Sep 26, 2022 03:37 UTC
  • Idadi ya vifo vya Ebola Uganda yafikia 21; maambukizo zaidi yaripotiwa

Idadi ya watu walioaga dunia nchini Uganda kwa maradhi hatari ya Ebola imeongezeka na kufikia 21 huku kukiweko na taarifa za kuenea kwa kasi maambukizo ya maradhi hayo.

Taarifa kutoka nchini Uganda zinasema kuwa, miji mingine kadhaa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki imeripoti kesi za maambukizo ya ebola na kuzua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi.

Serikali imetoa agizo kwa mamlaka husika hasa Wizara ya Afya kuchukua hatua za kuudhibiti ugonjwa huo sambamba na hatua zaidi za tahadhari kama kuwafuatilia watu waliokutana na wagonjwa wa maradhi hayo.

Wakati huo huo, mataifa ya Afrika Mashariki kama Kenya na Tanzania yametangaza umakini na kuchukua tahadhari katika mipaka yake na Uganda, kuhakikisha kuwa virusi hivyo havisambai.

Mlipuko wa ugonjwa Ebola mara ya mwisho ulitokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokkrasia ya Congo ambapo ulianza Agosti 2018 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,800.

 

Kumekuweko kwa milipuko minne nchini Uganda na mara ya mwisho Uganda iliripoti mlipuko wa maradhi hayo hatari mwaka 2021.

Ebola ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusababisha kifo na hupata binadamu na nyani. Ebola ina aina sita ya virusi, ambavyo vitatu kati yao ni Bundibugyo, Sudan na Zaire na vimeshasababisha milipuko.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.