Sep 27, 2022 04:37 UTC
  • Viwavi jeshi vyavamia mashamba ya mahindi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Wakulima wa zao la mahindi wanalia katika eneo la Nyiragongo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya viwavi jeshi kuvamia mashamba yao.

Mashamba hayo ya mahindi ambayo yanamilikiwa na jamii ya Munguiko yamekumbwa na uvamizi wa viwavi jeshi yaani (Armyworm); ambapo madhara yameripotiwa kuwa makubwa. Wadudu hao hushambulia majani na mashina ya mimea ya mahindi, hivyo basi hushindwa kukua au kufikia hatua ya kuchanua maua.

"Ni viwavi jeshi wanaoshambulia mashamba yetu. Wanatokea wakati wowote; iwe ni katika msimu wa  kiangazi au msimu wa mvua," ameeleza mkulima ambaye shamba lake limeharibiwa. Itakumbukwa kuwa katika miezi ya karibuni, viwavi jeshi walivamia mashamba ya mahindi huko Uganda, Zambia, Kenya na nchi nyinginezo barani Afrika. 

Jadot Mateso ambaye ni mtaalamu wa kilimo anasema kuwa, wadudu hao kitaalamu wanaitwa Spodoptera Frugitera, na  asili yao ni Amerika Kaskazini. Minyoo hao husababisha uharibifu mkubwa katika mashamba na wanaweza kupunguza uzalishaji wa kilimo kwa zaidi ya asilimia 60.

Uvamizi mkubwa wa viwavi jeshi mashambani 

Taathira za uvamizi wa viwavi jeshi zinaonekana katika masoko huko Goma ambapo bei ya mahindi imepanda kwa kiasi kikubwa kutokana na kupungua uzalishaji ulioathiriwa na wadudu hao. Georgette Nyabade mfanyabiashara wa mahindi katika mji wa Goma mashariki mwa Kongo anasema kuwa gunia la mahindi ambalo lilikuwa likiuzwa kwa dola za Kimarekani 30 hadi 35 sasa linauzwa dola 75 hadi 80. 

Viwavi jeshi ni wadudu wanaoharibu mazao katika maeneo ya kitropiki na yenye joto. Minyoo hao wenye njaa wanaweza kuharibu mashamba yote ya mazao kabla ya kuendelea na usakaji wao wa chakula zaidi, ambao husababisha athari mbaya za kiuchumi. Mahindi ni chakula kikuu kinachotumiwa pakubwa na wakazi wa maeneo ya mashariki mwa Kongo. Uvamizi wa viwaji jeshi katika eneo hilo umeibua hali ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa kukumbwa na tatizo la chakula katika mashariki mwa Kongo; eneo ambalo tayari limetumbukia katika machafuko ya waasi na makundi yanayobeba silaha. 

 

Tags