Sep 27, 2022 04:39 UTC
  • Libya:Watano wauawa katika mapigano kati ya makundi yenye silaha

Kundi la wanaume na wanawake waliokuwa na silaha walipigana usiku wa kuamkia jana Jumatatu katika mji wa Zawiya magharibi mwa Liba na kusababisha vifo vya watu watano. Watu wengine 13 walijeruhiwa katika mapigano hayo. Tarifa hizi ni kwa mujibu wa duru za huduma za dharura.

Mapigano hayo yaliyohusisha silaha nzito yalijiri baina ya makundi mawili yenye mfungamano rasmi na Wizara ya Ulinzi na Mambo ya Ndani za Libya katikati mwa mji wa Zawiya umbali wa kilomita 40 kutoka mji mkuu wa Libya, Tripoli. Idara ya Huduma kwa Wagonjwa ya Libya imearifu kuwa, watu 5 waliuawa akiwemo binti wa miaka 10. Watu 13 walijeruhiwa kwenye mapigano katika mji wa Zawiya magharibi wa Libya.

Mapigano hayo yaliibuka baada mwanachama mmoja kati ya makundi hayo mawili kuuawa na mfuasi wa kundi lal upande wa pili chanzo kikiwa ni wizi wa mafuta. Wizi wa mafuta limekuwa jambo la kawaida katika mji huo karibu na mpaka na Tunisia. Mapigano katika mji wa Zawiya magharibi mwa Libya yameripotiwa huku nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ikiwa imewathiriwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Serikali mbili zinazoiongoza nchi hiyo ambapo moja inaongozwa na Abdelhamid Dbeibah na nyingine na Fathi Bachagha  zimekuwa zikiwania madaraka  tangu mwezi Machi mwaka huu. Mapigano kati ya makundi hasimu ya wanamgambo yaliibuka huko Tripoli mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu na kusababisha atu 32 kupoteza maisha na 159 kujeruhiwa.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Libya ilitumbukia katika dimbwi la machafuko na hali ya mchafukoge baada ya kupinduliwa utawala wa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, na hivyo kuanza vita vya kuwania madaraka kati ya makundi na mirengo hasimu nchini humo. 

Kanali Muammar Gaddafi