Sep 27, 2022 08:11 UTC
  • Padri wa Kanisa Katoliki Tanzania afikishwa mahakamani kwa mashtaka ya ubakaji

Padri wa Kanisa Katoliki Kaskazini mwa Tanzania amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya ubakaji.

Sostenes Bahati Soka, Padri wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro jana alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za ubakaji na kudhalilisha watoto kingono.

Watoto hao ni wanafunzi wa kuanzia darasa la sita hadi kidato cha kwanza waliokuwa wakihudhuria mafundisho ya komunio ya kwanza na kipaimara.

Kesi ya kwanza ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha ambapo Padri akabiliwa na shtaka moja la kumbaka mtoto wa miaka 12.

Mshtakiwa huyo mwenye umri wa miaka 41 amekana shtaka hilo huku Wakili wa Serikali, Kasimu Nasiri akisema upelelezi umekamilika na Hakimu Salome ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, 2022 ambapo atafikishwa kusomewa maelezo ya awali.

Katika kesi nyingine, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya, Erasto Phily mshtakiwa huyo amesomewa shtaka moja la ubakaji wa mtoto.

 

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Charles Kitima amesema kuwa Kanisa litatoa ushirikiano ili haki ipatikane katika kesi hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni kumeripotiwa matukio mengi ya vitendo vya kunajisi na kubaka watoto vinavyofanywa na makasisi na mapadri wa kanisa katoliki hususan huko barani Ulaya.

Mwezi Oktoba mwaka jana Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis alisema kuwa, mlolongo wa matukio ya unyanyasaji wa kingono yaliyoripotiwa kufanywa na makasisi dhidi ya watoto ni fedheha kubwa kwa kanisa hilo.