Sep 27, 2022 10:52 UTC
  • Kumbukumbu za kuuawa shahidi Imam Ridha AS zafanyika nchini Mauritius

Programu maalumu ya kukumbuka siku alipouawa shahidi Imam Ridha AS zimefanyika nchini Mauritius na kuhudhuriwa na masheikh wawili kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa uratibu wa ubalozi wa Iran nchini Madagascar na Kitengo cha Kimataifa cha Haram ya Imam Ridha AS.

Masheikh Mahmoud Rezavandi na Mohsen Asadi wameongoza kumbukumbu hizo za kiroho, kiutamaduni na kimaanawi huko Mauritius.

Ni vyema tukakumbusha hapa kwamba, katika siku ya mwisho ya mwezi wa Mfunguo Tano, Safar miaka 1240 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha AS, mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW.

Imam Ridha AS alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS.

Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash'had Iran

 

Mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu.

Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia hofu Maamun, hivyo aliamua kumpa sumu na kumuua shahidi Imam Ridha katika siku kama leo.

Haram ya Imam Ridha AS iko katika mji wa Mash'had wa kaskazini mashariki mwa Irana na unavutia mamilioni ya wafanyaziara kila mwaka kutoka kona zote za dunia.

Tags