Sep 28, 2022 03:38 UTC
  • Askari 11 wauawa, raia 50 watoweka kufuatia shambulio la kigaidi Burkina Faso

Wanajeshi wasiopungua 11 wa Burkina Faso wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulio linaloaminika kuwa la kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo.

Hayo yaliripotiwa jana Jumanne na shirika la habari la Reuters ambalo limeeleza kuwa, msafara wa magari 150 ulishambuliwa na magaidi wanaobeba silaha katika mji mmoja wa kaskazini mwa nchi, na kupelekea askari 11 kupoteza maisha huku wengine kadhaa wakipata majeraha.

Habari zaidi zinasema kuwa, takriban raia 50 wametoweka kufuatia hujuma hiyo ya juzi Jumatatu. Inaarifiwa kuwa, msafara huo ulioshambuliwa ulikuwa ukipeleka misaada ya kibinadamu katika mji wa kaskazini mwa nchi.

Hii ni katika hali ambayo, mapema mwezi huu, raia 35 waliuawa na wengine 37 kujeruhiwa katika shambulio jingine la kigaidi dhidi ya msafara wa misaada ya kibinadamu huko kaskazini mwa Burkina Faso. 

Burkina Faso ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani na imekuwa ikikabiliana na waasi wa makundi ya kigaidi ya Daesh na al Qaida waliotokea nchi jirani ya Mali mwaka 2015. 

Mashambulizi ya waasi hao yamesababaisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha takriban watu milioni 1.9 kuyakimbia makazi yao.

Tags