Sep 28, 2022 08:06 UTC
  • Vikwazo vya Marekani vinazuia kupelekwa misaada ya kibinadamu Somalia

Shirika moja la kibinadamu limesema vikwazo vya Marekani vya 'kupambana na ugaidi' vimekwamisha shughuli za kuwafikishia wananchi wa Somalia misaada ya kibinadamu.

Mjumbe mwandamizi wa shirika hilo ambaye hakutaka kutaja jina lake ameliambia shirika la utangazaji la BBC kuwa, ingawaje wamefanikiwa kukusanya fedha walizohitaji na hata zaidi, lakini wameshindwa kuwafikishia wananchi wa Somalia misaada ya kibinadamu kutokana na sheria ya kupambana na ugaidi ya Marekani.

Afisa mwingine kutoka shirika jingine tofauti la misaada ya kibinadamu ambaye pia hakutaja jina lake ameashiria namna vikwazo hivyo vya Marekani vinavyozuia kufikishiwa misaada ya kibindamu Wasomali wanaohitaji, na kubainisha kuwa, 'Hatuwezi kupiga hata hatua moja mbele."

Marekani kwa upande wake inadai kuwa, inafahamu hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, na kwamba sheria zake za kupambana na ugaidi nchini Somalia, hazilengi kukwamisha misaada ya kibinadamu.

US inakwamisha kufikishiwa misaada Wasomali

Haya yanajiri wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, watu milioni nane wanakabiliwa na baa la njaa nchini Somalia, huku 213,000 miongoni mwao wakiwa katika hatari ya kufa njaa.

Nalo Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linakadiria kuwa, watoto milioni 3.6 huko Kenya, Somalia na Ethiopia wako katika hatari ya kuacha shule  kutokana na ukame ulioliathiri eneo la Pembe ya Afrika.

Tags