Sep 28, 2022 10:42 UTC
  • Wanajeshi wa Nigeria wakomboa mateka 7 katika jimbo Kaduna la kaskazini mwa nchi

Jeshi la Nigeria limesema kuwa, limefanikiwa kukomboa takriban watu saba waliokuwa wametekwa nyara na watu wenye silaha, katika operesheni ya hivi majuzi iliyofanywa na jeshi hilo kwenye jimbo la Kaduna la kaskazini mwa nchi hiyo.

Samuel Aruwan, kamishna wa usalama wa ndani wa jeshi la Nigeria amesema, wanajeshi wa Nigeria waliendesha operesheni hizo katika misitu iliyoko kati ya maeneo mawili ya Birnin-Gwari na Chikun katika jimbo hilo na walipambana vikali na baadhi ya magaidi wenye silaha.

Afisa huyo ameongeza kuwa, magaidi wengine walikimbia kuwaacha mateka na silaha nyuma.

Mateka hao saba wamerejea kwenye familia zao. Mashambulizi ya kutumia silaha yamekuwa tishio kubwa kwa usalama wa wananchi katika mikoa ya kaskazini na katikati mwa Nigeria.

Jeshi la Nigeria linaendesha operesheni za mara kwa mara dhidi ya magaidi

 

Mara kwa mara jeshi la Nigeria huwa linataka kuangamiza magaidi wenye silaha hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Mwenzi uliopita wa Septemba, jeshi la Nigeria lilitangaza habari ya kuwaangamiza mamia ya wanachama wa genge la kigadi la Boko Haram na lile la Daesh linalojiita ISIS Wilaya ya Afrika Magharibi (ISWAP) kaskazini mwa nchi hiyio.

Meja Jenerali Christopher Musa, Kamanda wa Kikosi cha Pamoja cha Kupambana na Ugaidi Kaskazini Mashariki mwa Nigeria alisema magaidi wasiopungua 420 waliuawa katika operesheni zilizofanyika mwezi Agosti katika jimbo la Borno. 

Alisema baadhi ya magaidi hao wameuawa licha ya kukimbilia katika vichaka na misitu ya karibu, baada ya ngome zao kusambaratishwa.

Meja Jenerali Musa aliongeza kuwa, operesheni hizo za kutokomeza ugaidi katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria zilihusisha wanajeshi wa nchi kavu pamoja na wa angani.