Sep 28, 2022 10:44 UTC
  • Vyama vya upinzani Sudan: Israel ndilo tishio kubwa kwa Sudan na ukanda huu wote

Vyama vya upinzani nchini Sudan vimesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndilo tishio kubwa kwa Sudan na kwa ukanda huu wote.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo leo Jumatano na kuvinukuu vyama hivyo vya Sudan vikilaumu vikali matamshi ya hivi karibuni ya Jenerali Abdel Fattah al Burhan, mkuu wa baraza la utawala la Sudan ambaye pia ndiye mkuu wa jeshi la nchi hiyo na kusema kuwa, al Burhan si mwakilishi wa wananchi wa Sudan. Wananchi wa Sudan wanaamini kwa dhati kwamba utawala wa Kizayuni ndilo tishio kwa Sudan na eneo hili lote.

Siddiq Tawer Kafi, mjumbe wa zamani wa baraza la uongozi la Sudan amesema: Matamshi ya mkuu huyo wa jeshi la Sudan yanawakilisha tu msimamo wa serikali ya majenerali wa kijeshi waliofanya mapinduzi na ambao wanang'ang'ania madaraka ya Sudan kinyume cha sheria. Matamshi hayo ni katika ndoto na matakwa binafsi ya Jenerali Abdel Fattah al Burhan.

Jeneral Abdel Fattah al Burhan anayependa kujikomba kwa Wazayuni

 

Naye Adil Khalafallah, mmoja wa viongozi wa harakati ya ukombozi na mabadiliko ya Sudan amesema, matamshi ya Jenerali Burhan ni matamshi yake binafsi na hayawakilishi msimamo wa wananchi wa Sudan. Amesema, Burhan anajaribu kunadi na kuuza mitazamo yake kwa wale tu wanaopenda kununua mitazamo kama hiyo hata kama ni utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Abdel Fattah al Burhan, mkuu wa baraza la utawala linalotawala Sudan hivi sasa alisema, huenda hivi karibuni akautembelea utawala wa Kizayuni kwani amedai uhusiano wa Sudan na Israel ni wa maelewano.