Sep 29, 2022 02:25 UTC
  • Mtawala wa zamani wa kijeshi wa Guinea afikishwa mahakamani kwa mauaji ya 2009

Rais na mtawala wa zamani wa kijeshi wa Guinea, Moussa Dadis Camara na wenzake 10 wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya mauaji yaliyofanyika katika uwanja wa michezo mjini Conakry hapo 2009 na ubakaji mkubwa uliofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Watuhumiwa hao 11 wanakabiliwa na mashtaka ya kuhusika na mauaji ya zaidi ya watu 150 na ubakaji wa wanawake zaidi ya 100 katika mji mkuu, Conakry, kulingana na ripoti ya tume ya kimataifa iliyopewa mamlaka na Umoja wa Mataifa.

Tarehe 28 Septemba 2009, makumi ya maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia walifanya maandamano katika uwanja wa michezo mjini Conakry ili kumshinikiza Camara asigombee uchaguzi wa rais wa Guinea mwaka uliofuata. Camara aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 2008.

Manusura wa mauaji hayo wamezungumzia jinsi kulivyotokea mauaji ya kutisha huku wahasiriwa wengine wakipigwa risasi. Wanawake na wasichana walipigwa na kubakwa na vikosi vya usalama.

Watu walioshuhudia wameeleza kwamba, walinzi wa rais, maafisa wa polisi na wanamgambo waliingia uwanjani mwendo wa saa sita mchana, wakafunga njia zote za kutoka na kufyatua risasi kiholela dhidi ya umati wa watu. Raia wa kawaida walishambuliwa kwa visu, mapanga na mikuki, na kuacha makumu ya maiti za watu zikiwa zimetapakaa ovyo. Watu wengine walikanyagwa hadi kufa kwa hofu.

Guinea

Wachunguzi wa kimataifa wanasema unyanyasaji huo unaweza kutambuliwa kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, wakisisitiza kuwa ukatili huo uliendelea kwa siku kadhaa dhidi ya wanawake na wanaume waliokuwa wakipewa mateso.

Camara amekanusha kuhusika na tukio hilo, akiwalaumu askari waliofanya makosa, akiwemo msaidizi wake wa zamani Luteni Aboubacar Toumba Diakite, ambaye pia ni miongoni mwa waliofunguliwa mashtaka.