Sep 29, 2022 08:02 UTC
  • Kenya yazidisha hatua za kufuatilia kesi za Ebola katika mpaka wake na Uganda

Maafisa wa Afya katika mji wa Busia wamezidisha jitihada za kuwapima na kufuatilia kesi za maambukizi ya ugonjwa wa Ebola ikiwa ni katika juhudi za kuzuia msambao wa virusi vya ugonjwa huo katika maeneo ya mpakani.

Wamesema kuwa, kila mtu anayepita katika eneo la mpaka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Sudan Kusini, na Uganda kuelekea Kenya sasa lazima afanyiwe uchunguzi kwenye kivuko cha mpakani.

Dakta Melsa Lutomia Kaimu Afisa wa Afya katika serikali ya kaunti ya Busia ameeleza kuwa, watu  wanaovuka mpaka kwanza wanapimwa joto la mwili na kusajiliwa kwenye fomu husika. "Kimsingi wanajaza maelezo yao ya kibinafsi kama vile jina na mawasiliano yao na walikoanzia safari ili tuweze kutambua kama wanatoka maeneo yoyote karibu na tarafa ya Mubende nchini Uganda" amesema Dakta Lutomia.

Ameongeza kuwa, kama  joto la mwili wa mtu limeonekana kupindukia nyuzi joto 37.8 wanawaelekeza katika chumba husika cha mapokezi mpakani kwa ajili ya uchunguzi zaidi. 

Hatua za kubaini kesi za Ebola katika mpaka wa Uganda 

Hata hivyo maafisa wa mpakani wanasema kuwa, hawajabaini mtu mwenye maambukizi licha ya kwamba hadi sasa wamewapima watu zaidi ya 5000 tangu kuripotiwa kesi ya kwanza ya Ebola huko Uganda wiki mbili zilizopita. 

 

Tags