Sep 29, 2022 12:21 UTC
  • Kabuga, mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda akwepa ufunguzi wa kesi yake

Felicien Kabuga anayetuhumiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda ameripotiwa kukataa kuhudhuria ufunguzi wa kesi dhidi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya mjini Hague nchini Uholanzi.

Hayo yamesemwa leo Alkhamisi na majaji wa mahakama hiyo ambao hata hivyo wamesisitiza kuwa, kesi dhidi ya Kabuga anayekabiliwa na mashitaka matatu ya mauaji ya kimbari itaendelea kuanzia leo, licha ya kutokuwepo kwake mahakamani.

Rashid S. Rashid, Mwendesha Mashitaka wa ICC amesema "Miaka 28 baada ya matukio (ya mauaji ya kimbari), kesi hii ina lengo la kumbebesha dhima Felicien Kabuga kutokana na nafasi yake katika mauaji ya kimbari."

Hapo awali majaji wa ICC walisema kuwa, Kabuga ataruhusiwa kuhudhuria vikao hivyo kwa njia ya vídeo kama italazimika kufanya hivyo, kwa sababu ya hali yake ya kiafya.

Kabuga alikamatwa tarehe 16 Mei mwaka 2020 katika kitongoji kimoja mjini Paris, baada ya kukaa mafichoni kwa miaka 25. Anatuhumiwa kusaidia kuunda kundi la wanamgambo wa Interahamwe, kundi kuu lenye silaha ambalo lilihusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 800,000 kulingana na Umoja wa Mataifa.

Kabuga ni mmoja wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda

Kabuga ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu alikuwa mwanachama wa kundi linalojulikana kama Akazu, ambalo linadaiwa kuhusika katika kueneza itikadi na kusimamia mauaji ya kimbari ambayo yalipelekea Watutsi karibu milioni moja kuuawa.

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalitokea kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Tags