Sep 29, 2022 13:34 UTC
  • Rais Museveni: Uganda haitatekeleza karantini kufuatilia mlipuko wa maradhi ya Ebola

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ameondoa wasiwasi kwa umma unaodhani kwamba, angetangaza hatua za karantini katika hatua za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola katika nchi hiyo.

Akihutubia taifa, kiongozi huyo amelezea kuwa hapana haja ya kuweka vizuizi kwa sababu ameona pana urahisi kudhibiti maambukizi ya Ebola ikilinganishwa na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

Kiongozi huyo wa Uganda amesema kwenye hotuba yake kwamba kulingana na takwimu za Wizara ya Afya ni watu watano ndiyo wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na mlipuko wa Ebola tangu wizara hiyo ilipotangaza rasmi kwamba, ugonjwa huo umegunduliwa nchini Uganda. Waathirika kwa jumla ni 31 na kwamba kwa sasa idadi kubwa ya waathirika wamo katika wilaya tatu zilizo jirani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, ugonjwa wa Ebola ulioznzia Sudan umeonesha kuwa hauambukizi kwa kasi na pia kiwango cha vifo ni cha chini tofauti na milipuko ya hapo awali iliyotokea nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo karibu watu 2,300 walikufa mnamo mwaka 2018 hadi mwaka 2020.

 

 

Huko nchini Uganda maambukizi ya hivi karibuni yalizuka katika wilaya ya Mubende katikati mwa Uganda, karibu kilomita 150 magharibi mwa mji mkuu Kampala na tangu wakati huo yameenea katika wilaya mbili zaidi.

Akitangaza uamuzi wa kutotekeleza sheria ya karantini, Rais Museveni amefafanua kuwa amefanya maamuzi hayo kwa ushauri wa wataalamu wa afya na wanasayansi na amewaaambia raia wake kwamba ni rahisi kuepusha maambukizi ya Ebola ikiwa watazingatia usafi wa mwili na kwenye maeneo yao na kuwahimiza kuosha mikono mara kwa mara.