Sep 30, 2022 11:14 UTC
  • Mahakama ya Zimbabwe yampiga faini mwandishi wa riwaya kwa kuchochea maandamano

Mwandishi wa vitabu na mtayarishaji filamu wa Zimbabwe, Tsitsi Dangarembga ametozwa faini na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya mahakama kumpata na hatia ya "kuchochea ghasia za umma" wakati wa maandamano ya kupinga serikali ya 2020.

Dangarembga amehukumiwa pamoja na rafiki yake na muandamanaji mwenzake Julie Barnes, ambaye pia amepatikana na hatia.

Wawili hao wametozwa faini ya dola 70,000 za Zimbabwe ($193) na kupewa adhabu ya kifungo, ambayo ina maana kwamba watakuwa huru iwapo hawatatenda kosa kama hilo katika miaka mitano ijayo.

Mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa, Dangarembga amekuwa akipigana kwa miaka mingi dhidi ya ufisadi na kutoa wito wa marekebisho. Amesisitiza wakati wa kesi yake kwamba Wazimbabwe wana haki ya kufanya maandamano.

Hakimu wa mahakama ya Harare, Barbara Mateko, amesema "Wawili hao walinuia kuchochea ghasia na wamepatikana na hatia kama walivyoshtakiwa."

Dangarembga mwenye umri wa miaka 63 amesema "hakushangazwa" na uamuzi huo.

Dangarembga na Barnes walikamatwa mwishoni mwa Julai 2020 baada ya kuandamana katika mjini Harare, wakiwa wameshikilia mabango yenye maandishi yanayoikosoa serikali.

Wanasheria wa haki za binadamu wanasema makumi ya wanaharakati walikamatwa na vikosi vya usalama vilivyotumwa kuzima maandamano hayo. Wanasheria wa haki pia walisema kulishuhudiwa visa vya utekaji nyara na utesaji, jambo ambalo serikali imelikanusha.