Sep 30, 2022 11:46 UTC
  • Milio ya risasi nzito, wanajeshi mitaani katika mji mkuu wa Burkina Faso

Habari kutoka mjini mkuu wa Burkina Faso zinasema kuwa, wanajeshi wako mitaani na milio ya risasi imesikika karibu na kambi kuu ya kijeshi na maeneo ya makazi ya raia kwenye mji mkuu Ouagadougou. Mripuko mkubwa pia umesikika leo Ijumaa karibu na Ikulu ya Rais na wanajeshi wamewekwa kwenye tahadhari kubwa.

Wanajeshi wameonekana kwenye njia kuu inayoelekea Ikulu ya Rais na kwenye majengo ya utawala na kituo cha televisheni cha taifa, ambacho kimesitisha matangazo. Waandishi wa habari wamesema pazia jeusi ndilo lililotanda kwenye televisheni ya taifa likiwa na ujumbe unaosema: "hakuna mawimbi ya video."

Barabara kuu kadhaa mjini Ouagadougou zimefungwa na wanajeshi. Msemaji wa serikali ya kijeshi iliyonyakua madaraka mwezi Januari mwaka huu hakuweza kupatikana ili kutoa maelezo kuhusu kinachoendelea. 

Haijajulikana bado kama hilo lilikuwa ni jaribio la mapinduzi au la, lakini dalili zote zimeonesha kutokea mapinduzi mengine ya kijeshi yaliyoikumbwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kwa mara kadhaa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. 

Wanajeshi wakiwa wamejizatiti mjini Ouagadougou Burkina Faso

 

Ghasia zimeendelea nchini Burkina Faso tangu Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba alipotwaa madaraka katika mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Januari, na kumuangusha kiongozi aliyechaguliwa na wananchi, Roch Marc Christian Kabore.

Matukio ya leo Ijumaa yamekuja siku mbili baada ya serikali ya Burkina Faso kusema kuwa wanajeshi 11 wameuawa na raia 50 hawajulikani walipo baada ya watu wenye silaha kushambulia msafara wa magari 150 uliokuwa na wanajeshi waliokuwa wanapeleka vifaa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne, serikali ya Burkina Faso ilisema, shambulio hilo lilifanyika Jumatatu katika wilaya ya Gaskinde ya mkoa wa Soum, wa kaskazini mwa nchi hiyo.