Oct 01, 2022 05:29 UTC
  • Kiongozi wa kijeshiBurkina Faso Damiba aondolewa madarakani na wanajeshi

Kapteni katika Jeshi la Burkina Faso Ibrahim Traore amemuondoa madarakani mtawala wa kijeshi Paul-Henri Damiba, kuivunja serikali na kusimamisha katiba na hati ya serikali ya mpito.

Katika taarifa yake iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa Ijumaa jioni, Traore alisema kwamba kundi la maafisa waliamua kumwondoa madarakani Damiba kutokana na kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na ghasia na hujuma za kigaidi zinazozidi kuwa mbaya nchini humo.

Hii ni mara ya pili kwa jeshi kufanya mapinduzi ndani ya miezi minane kwa taifa hilo la Afrika Magharibi. Damiba alinyakua mamlaka katika mapinduzi ya Januari ambayo yalimpindua Rais wa zamani Roch Kabore, pia kutokana na hali mbaya ya ukosefu wa usalama.

Burkina Faso imekuwa ikijitahidi kuzuia makundi ya waasi, yakiwemo yale yanayohusishwa na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh au ISIS.

Huku asilimia 40 ya Burkina Faso ikiwa nje ya udhibiti wa serikali, kumeshuhudiwa hali ya kutoridhika na hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na magaidi na waasi.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ililaani vikali mapinduzi hayo siku ya Ijumaa, ikisema kwamba yalikuja katika wakati "usiofaa" ambapo maendeleo yalikuwa yakifanywa kuelekea kurejea kwa utaratibu wa kikatiba.

katika taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ECOWAS imebainisha upinzani wake kwa unyakuzi wowote au udumishaji wa mamlaka kwa njia zisizo za kikatiba.

Siku ya Ijumaa, Traore alitangaza kwamba mipaka ya nchi itafungwa kwa muda usiojulikana na kwamba shughuli zote za kisiasa na mashirika ya kiraia zimesitishwa. Amri ya kutotoka nje kutoka saa tatu usiku hadi  saa 11 alfajiri pia imetangazwa.

"Tukiwa tumekabiliwa na hali mbaya, tulijaribu mara kadhaa kumshauri Damiba kuangazia upya suala la usalama," ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Traore na kusomwa na afisa mwingine kwenye televisheni, akisindikizwa na kundi la askari waliokuwa wamevalia sara za kijeshi huku wakiwa wamejizatiti kwa silaha.

Taarifa hiyo imesema Damiba alikataa mapendekezo ya maafisa hao ya kupanga upya jeshi na badala yake kuendelea na muundo wa kijeshi uliosababisha kuanguka kwa serikali iliyopita.

Mashambulizi ya kigaidi yameongezeka tangu katikati ya mwezi Machi, licha ya ahadi ya serikali ya kijeshi kufanya usalama kuwa kipaumbele chake kikuu.