Oct 01, 2022 06:08 UTC
  • Ajali zaua watu 145 nchini Kenya ndani ya wiki moja

Watu wasiopungua 145 wamepoteza maisha katika matukio tofauti ya ajali za barabarani nchini Kenya ndani ya siku saba zilizopita.

Takwimu hizo za kuogofya zilitangazwa jana Ijumaa na Idara ya Polisi nchini humo (NPS) ambayo imeeleza kuwa, ubovu wa magari, ulevi, upuuzaji wa sheria za barabarani na kuendesha magari kwa mwendo wa kasi ni miongoni mwa mambo yanayochangia kushuhudiwa ajali hizo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Aidha ajali mbaya za magari hutokea mara kwa mara nchini Kenya, ambako barabara nyingi kuu ni nyembamba na aghalabu yazo zimejaa mashimo.

Kwa wastani, Wakenya 3,000 hupoteza maisha kila mwaka katika ajali za barabarani. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA).

Ajali Kenya

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa, duniani kote ajali za barabarani zinaua watu takriban milioni 1.3 kila mwaka ambao ni sawa na zaidi ya watu wawili kila dakika, huku wengine milioni 50 wakijeruhiwa.

Aidha takwimu hizo zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 90% ya vifo hivyo au vifo 9 kati ya 10 vinatokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Tags