Oct 01, 2022 12:14 UTC
  • Daktari Mtanzania aaga dunia kwa Ebola nchini Uganda

Daktari mmoja raia wa Tanzania aliyekuwa akifanya kazi nchini Uganda ameaga dunia kutoka na ugonjwa wa Ebola.

Hayo yametangazwa leo Jumamosi na Dakta Jane Ruth Aceng, Waziri wa Afya wa Uganda ambaye ameeleza kuwa, hiki ndicho kifo cha kwanza cha daktari, na mfanyakazi wa afya wa pili kupoteza maisha kwa maradhi hayo katika mripuko wa sasa nchini humo.

Amesema Dakta Mohammed Ali aligunduliwa kuwa ameambukizwa ugonjwa huo mnamo Septemba 26, na ameaga dunia alfajiri ya leo akitibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Fort Portal nchini humo.

Chama cha Madaktari wa Upasuaji Uganda kimethibitisha pia Dakta Mohammed Ali, Mtanzania aliyekuwa na umri wa miaka 37 ameaga dunia kwa maradhi ya Ebola, ingawaje hakijaeleza namna alivyoambukizwa virusi hivyo. 

Chama hicho kimesema raia huyo wa Tanzania alikuwa anasomea shahada ya uzamili katika fani ya upasuaji katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala.

Ebola DRC; Mripuko wa sasa umemalizika

Idadi ya watu walioaga dunia nchini Uganda kwa maradhi hayo hatari imeripotiwa kuongezeka na kufikia 24, wakati huu ambapo kuna taarifa za kuenea kwa kasi maambukizo ya maradhi hayo nchini humo. Licha ya msambao huo, lakini Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ameondoa wasiwasi kwa umma unaodhani kwamba, angetangaza hatua za karantini katika hatua za kudhibiti mripuko wa ugonjwa huo hatari katika nchi hiyo.

Nchi za kanda ya Afrika Mashariki hususan zinazopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimechukua hatua za tahadhari za kukabiliana na msambao wa Ebola.

 

 

Tags