Oct 02, 2022 08:02 UTC
  • AU yalaani mapinduzi ya kijeshi Burkina Faso, Ufaransa yatuhumiwa kuhusika

Umoja wa Afrika (AU) umelaani hatua ya 'wanajeshi waasi' kutwaa mamlaka ya nchi kinyume cha katiba huko Burkina Faso, katika hali ambayo nchi hiyo ilikuwa katika mkondo wa kurejesha utawala wa kiraia.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU amesema katika taarifa kuwa, anatiwa wasiwasi na kurejea kwa wimbi la mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, na mataifa mengine ya bara hilo.

Taarifa ya AU imesema: Mwenyekiti (wa Kamisheni ya AU) anatoa mwito kwa jeshi (la Burkina Faso) kujiepusha mara moja na hatua za ghasia au zinazoweza kutishia usalama wa raia, uhuru wa kiraia na haki za binadamu.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ametoa mwito wa kurejeshwa utawala wa kikatiba nchini Burkina Faso kufikia Julai mwaka 2024 kama ilivyokuwa imeratibiwa kwenye mpango wa amani wa nchi hiyo.

Kabla ya hapo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) ilieleza bayana kuwa, hatua ya wanajeshi hao kumuondoa madarakani mtawala wa kijeshi Paul-Henri Damiba ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

Ijumaa jioni, Kapteni katika Jeshi la Burkina Faso Ibrahim Traore alitangaza kumuondoa madarakani mtawala wa kijeshi Paul-Henri Damiba, kuivunja serikali na kusimamisha katiba na hati ya serikali ya mpito. Katika taarifa yake iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, Traore alisema kwamba kundi la askari limeamua kumwondoa madarakani Damiba kwa kushindwa kukabiliana na ghasia na hujuma za kigaidi zinazozidi kuwa mbaya nchini humo.

Hii ni mara ya pili kwa jeshi kufanya mapinduzi ndani ya miezi minane kwa taifa hilo la Afrika Magharibi. Damiba alinyakua mamlaka katika mapinduzi ya Januari ambayo yalimpindua Rais wa zamani Roch Kabore, pia kutokana na hali mbaya ya ukosefu wa usalama.

Mahamat (kushoto), na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres aliyelaani pia mapinduzi ya Burkina Faso

Wakati huohuo, kundi la jeshi lililofanya mapinduzi Ijumaa linasema, Luteni Kanali Paul-Henri Damiba aliyepinduliwa amejificha katika kambi ya jeshi ya Ufaransa katika eneo la Kamboinsin mjini Ouagadougou, na kwamba anapanga kufanya shambulizi dhidi ya wafanyamapinduzi kutoka eneo hilo.

Hata hivyo, ubalozi wa Ufaransa mjini Ouagadougou umekanusha madai kuwa serikali ya Paris imehusika kwenye mapinduzi hayo. Aidha Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imedai kuwa, si ubalozi wala kambi hiyo yenye wanajeshi wa Ufaransa imemkaribisha Damiba.

Wanajeshi waitifaki wa Paul-Henri Damiba wamepuuza madai ya kujiri mapinduzi, wakisisitiza kuwa kilichotokea ni mvutano tu ndani ya jeshi hilo.

Tags