Oct 02, 2022 12:04 UTC
  • Ubalozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso washambuliwa, Paris inatuhumiwa kumficha Kanali Damiba

Ubalozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso umeshambuliwa baada ya Paris kushutumiwa kwamba imempa hifadhi kamanda wa jeshi la Burkina Faso, Luteni Kanali Paul-Henri Damiba aliyeng'olewa madarakani.

Waandamanaji waliokuwa na hasira wa Burkina Faso walivamia ubalozi wa Ufaransa huko Ouagadougou, jana Jumamosi baada ya Ufaransa kushutumiwa kwamba imempa hifadhi mkuu wa jeshi la Burkina Faso, Paul Henri Sandaugu Demiba.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imekanusha tuhuma za kuhusika katika machafuko ya sasa nchini Burkina Faso na kulaani shambulio lililolenga ubalozi wa nchi hiyo mjini Ouagadougou. Taarifa ya wizara hiyo imesema kwamba Paul Henri Sandaugu hayupo kwenye kambi ya kijeshi ya Ufaransa au ubalozi wa nchi hiyo huko Burkina Faso. 

Hata hivyo kundi la jeshi lililofanya mapinduzi linasema, Luteni Kanali Paul-Henri Damiba aliyepinduliwa amejificha katika kambi ya jeshi ya Ufaransa katika eneo la Kamboinsin mjini Ouagadougou, na kwamba anapanga kufanya shambulizi dhidi ya wafanyamapinduzi kutoka eneo hilo.

Kanali Paul-Henri Damiba

Ijumaa jioni, Kapteni katika Jeshi la Burkina Faso, Ibrahim Traore alitangaza kumuondoa madarakani mtawala wa kijeshi Paul-Henri Damiba, kuivunja serikali na kusimamisha utekelezaji wa katiba na hati ya serikali ya mpito. Katika taarifa yake iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, Traore alisema kwamba kundi la askari limeamua kumwondoa madarakani Damiba kwa kushindwa kukabiliana na ghasia na hujuma za kigaidi zinazozidi kuwa mbaya nchini humo.

Tags