Oct 03, 2022 10:24 UTC
  • 14 wauawa katika shambulio nchini Congo DRC

Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa, raia 14 wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika eneo moja kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia mgogoro kati ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi kwa muda wa miaka 20 iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti, raia 14 waliuawa Jumamosi usiku baada ya kutokea shambulio la silaha kwenye eneo la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kulingana na vyanzo vya ndani, wapiganaji wenye silaha wa muungano wa vikosi vya demokrasia walishambulia kabila moja katika mkoa wa Ituri, na kuua watu 14 kwa mapanga, kujeruhi wengine wawili na kuchoma moto nyumba 36. Mkuu wa kabila hilo alitangaza kuwa wahanga wa tukio hilo walizikwa kwenye kaburi la pamoja. Vyanzo vya ndani vinasema huenda sababu ya kutokea mashambulio kama hayo ni kutokuwepo vikosi vya kijeshi vya kutosha katika mkoa huo, ambao hushuhudia shughuli nyingi za makundi yenye silaha.

Wakimbizi wa vita DRC

Vikosi vya Democratic Alliance vimekuwa vikifanya uhalifu nchini Kongo kwa miaka mingi.

Vijiji vya Kongo hushambuliwa mara kwa mara na kuporwa na wanamgambo wa muungano huo wa waasi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, makundi ya waasi yenye silaha yaliwaua zaidi ya raia 1,200 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri mwaka uliopita.

Mauaji hayo ya mara kwa mara husababisha kutawanyika familia ambazo hukimbilia usalama wao katika maeneo tofauti ya nchi na hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.