Oct 04, 2022 02:17 UTC
  • Wafanyakazi 65 wa afya wawekwa karantini nchini Uganda kwa Ebola

Wizara ya Afya ya Uganda imetangaza kuwa imewaweka kwenye karantini wafanyakazi wasiopungua 65 wa afya baada ya wafanyakazi hao kushughulikia wagonjwa wa Ebola.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Uganda, Emmanuel Ainebyoona, amesema hayo na kuongeza kuwa, wafanyakazi watakaobainika wameambukizwa Ebola, watalazimishwa kubakia nyumbani kwa muda wa siku 21.

Ainebyoona pia amesema: Tumewaweka wafanyakazi wote hao kwenye karantini kwa ungalizi maalumu wa kimatibabu kwa muda wa siku 21. Tunaamini kuwa wamekutana na baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa na ugonjwa wa Ebola.

"Tumewaweka kwenye karantini watu hao lakini majumbani kwao, chini ya uangalizi wetu wa karibu. Mambo yote yanakwenda vizuri," amesema.

Dakta Mohammed Ali, Mtanzania aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda

 

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya daktari mmoja raia wa Tanzania anayejulikana kwa jina la Dakta Mohammed Ali kufariki dunia siku ya Jumamosi kwa ugonjwa wa Ebola katika wilaya ya Kabarole ya magharibi mwa Uganda.

Ugonjwa wa Ebola ulizuka tena nchini Uganda tarehe 20 mwezi uliopita wa Septemba, baada ya mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 24 kubainika kukumbwa na ugonjwa huo.

Siku 10 baadaye yaani tarehe 30 Septemba, Wizara ya Afya ya Uganda ilitangaza kuwa imesajili wagonjwa 38 waliothibitishwa kukumbwa na ugonjwa wa Ebola na vifo vya watu wanane. 

Takwimu za mwisho za ugoinjwa huo zinasema kuwa, watu walioaga dunia nchini Uganda kwa Ebola wameongezeka na kufikia 24, wakati huu ambapo kuna taarifa za kuenea kwa kasi maambukizo ya maradhi hayo nchini humo. 

Nchi za kanda ya Afrika Mashariki hususan zinazopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimechukua hatua za tahadhari za kukabiliana na msambao wa Ebola.